FERWAFA yathibitisha Super Cup 2026 ya timu nne bila APR FC, mabingwa wa Ligi na Peace Cup msimu uliopita
Na Christopher Karenzi
Baada ya APR FC kujiondoa katika mashindano ya Turbo King Super Cup 2026, Shirikisho la Soka nchini Rwanda (FERWAFA) limeamua kwamba Mukura Victory Sports & Loisirs ichukue nafasi ya timu hiyo.
Uamuzi huo ulitangazwa Jumanne, tarehe 18 Agosti 2026, baada ya FERWAFA kufanya mazungumzo mbalimbali na timu za APR FC, Rayon Sports, Kiyovu Sports na Police FC. FERWAFA ilisema: “Imeamuliwa kwamba Super Cup 2026 itachezwa na timu nne, katika mechi mbili za nusu fainali na mechi ya fainali, kama ilivyopangwa awali.”
“Ikizingatiwa kuwa APR FC iliijulisha FERWAFA kwamba haitashiriki mashindano haya kwa mfumo wa timu nne, imeamuliwa kwamba Mukura Victory Sports & Loisirs, iliyomaliza nafasi ya tano katika BK Pro League msimu wa 2025/2026, ndiyo itakayoshiriki mashindano haya kama timu ya nne.”
Mechi za nusu fainali zitachezwa Alhamisi, tarehe 27 Agosti 2026, katika Kigali Pelé Stadium. Kwanza itacheza Kiyovu Sports dhidi ya Mukura Victory Sports & Loisirs, kishaRayon Sports dhidi ya Police FC. Fainali pamoja na hafla ya kukabidhi kombe itafanyika Jumapili, tarehe 30 Agosti 2026, katika Kigali Pelé Stadium. Kila timu itakayoshiriki itapokea fedha za ushiriki, huku zawadi kwa bingwa na mshindi wa pili zikiwa zimeongezwa.
APR FC, ambayo haitashiriki mashindano haya, ndiyo bingwa mtetezi. Mwaka uliopita ilipokea faranga milioni 20 za Rwanda (Frw), huku Rayon Sports FC, iliyomaliza nafasi ya pili, ikipokea Frw milioni 10.

Mukura Victory Sports imechukua nafasi ya APR kwenye shindano la Super Cup 2026
APR FC inaeleza kuwa haikuwahi kupewa taarifa mapema kwamba mfumo wa mashindano hayo ungebadilishwa, jambo ambalo lingeisaidia kupanga maandalizi yake ya msimu wa 2026/27. Wakati uamuzi wa kubadilisha mfumo wa mashindano ulipokuwa ukifanywa, APR FC haikuitwa kama mwanachama anayehusika na mashindano hayo ili ishiriki katika kufanya uamuzi huo, pamoja na kufahamu manufaa yake kwa timu na kwa soka la Rwanda.
Kulingana na Msemaji wa APR FC, Tony Kabanda, klabu hiyo inaandaa mkutano na waandishi wa habari ambao utazungumzia sababu zilizoifanya kujiondoa katika mashindano ya FERWAFA Super Cup 2026, pamoja na masuala mengine yanayohusu soka

APR FC
Pia, APR FC inasema wanachama wote wa FERWAFA walipaswa kuitwa, kwa kuwa si timu nne pekee zinazohusika na mashindano ya Super Cup. Kwa kawaida, mashindano hayo huwakutanisha timu zilizofanya vizuri zaidi katika msimu uliopita. Walipopewa taarifa kuhusu uamuzi huo, walikuta APR FC tayari ilikuwa imepanga mechi za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya CAF Champions League 2026/27.
