Ferwafa kusimamisha waamuzi kutokana na mwenendo usiofaa
Na Christopher Karenzi
Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) limemsimamisha mwamuzi msaidizi Nsengiyumva Jean Paul kwa miezi 12 “kutokana na mwenendo usiofaa.”
Mwamuzi huyo wa pembeni pia amesimamishwa mechi tano kwa kushindwa kuongoza mchezo ipasavyo.
Wakati huohuo, Nshimiyimana Remy Victor aliyekuwa mwamuzi wa kati katika mchezo uliowakutanisha Mukura VS na Rutsiro FC Jumapili, naye amesimamishwa mechi tano kutokana na kuonyesha kiwango cha chini katika uamuzi.
Maamuzi haya yalifikiwa baada ya Kamati ya Usimamizi wa Waamuzi kukutana Jumatatu, tarehe 4 Mei 2026, na kuchambua michezo ya siku ya 29 ya BK Pro-League, hususan mchezo uliochezwa Huye kati ya Mukura VS na Rutsiro FC tarehe 03/05/2026.
Kamati hiyo ilisema ilizingatia kanuni za mwenendo wa waamuzi nchini Rwanda (Règlement du Statut d’Arbitrage 2026), ripoti ya kamishna pamoja na picha za video za mchezo.
Kamati ilikosoa uamuzi wa Nshimiyimana Rémy Victor, mwamuzi wa kati, na kumfungia mechi tano.
Mwamuzi huyo alikosea kwa kutoa penalti mbili zisizo sahihi kwa timu ya Rutsiro FC na kushindwa kusimamia mchezo kwa ujumla kama ilivyotakiwa.
Nsengiyumva Jean Paul, aliyekuwa mwamuzi msaidizi wa pili, alionekana kuwa na mwenendo usiofaa usioendana na majukumu yake, hivyo kupewa adhabu ya kusimamishwa miezi 12.
Kamati hiyo pia ilieleza kuwa maamuzi yasiyo sahihi ya kiufundi yaliathiri matokeo ya mwisho ya mchezo, hivyo akaadhibiwa kwa kusimamishwa mechi tano.

Nsengiyumva (wa kwanza kushoto) na Nshimiyimana (wa tatu kutoka kulia) wamesimamishwa kutokana na yaliyotokea katika mchezo kati ya Mukura VS na Rutsiro FC.
