Rais Kagame: Kwa nini Afrika daima ibaki nyuma?

Share Now

Na Christopher Karenzi

chriskarenzi@gmail.com

Rais Kagame amesema kuwa vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwekwa kwa baadhi ya nchi, ikiwemo Rwanda, si vya haki, kwa sababu mara nyingi huwekwa kwa kuzingatia maslahi ya mataifa yenye nguvu kutokana na ahadi au manufaa yanayotolewa kwao.

Rais Kagame  ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanya na mwanahabari wa CNN, Eleni Giokos, tarehe 14  mei 2026  katika  Kongamano la Wakurugenzi wakuu  Africa CEO Forum lilionza tarehe 14-15 mei 2026.

Lengo kuu la kongamano hili ni kujadili namna ya kukuza uchumi wa Afrika kupitia: Biashara na uwekezaji, ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi,ubunifu na teknolojia, ajira na maendeleo ya vijana, miundombinu na viwanda  pamoja na masuala ya fedha na maendeleo endelevu.

Zaidi ya viongozi 2,800 walhudhuria mkutano huo, wakiwemo marais wa nchi mbalimbali pamoja na wakurugenzi wa kampuni kubwa kutoka Afrika na maeneo mengine duniani. Jumla ya nchi 69 zilishiriki mkutano huo.

Rais wa Jamhuri ya Rwanda Paul Kagame

Rais Kagame alipoulizwa kuhusu vikwazo na mashinikizo vinavyowekwa kwa nchi za Afrika, amesema kuwa hali hiyo haiikumbi Rwanda pekee, bali mataifa mengine pia, na mara nyingi huamuliwa kwa kuzingatia maslahi ya baadhi ya nchi: Vikwazo huwekwa kwa kuzingatia nani anatoa kidogo au zaidi, na huishia kunufaisha yule anayetoa zaidi. Ikiwa mtu anajua atapata faida kubwa mahali fulani, ataipendelea sehemu hiyo hata kama walio huko ndio wenye makosa.”

Rais Kagame amesema kuwa changamoto zinazoikumba dunia kwa sasa zinapaswa kuikumbusha Afrika wajibu wake pamoja na mchango wake. Ameuliza kwa nini Afrika daima ibaki nyuma?” 

Rais Kagame amesema kuwa shinikizo linalowekwa kwa Afrika lina lengo la kuikumbusha kuwa inapaswa kuamka, kujitathmini, kutazama rasilimali ilizonazo, na kufanya yale yanayostahili ili iweze kupata nafasi yake ya pekee katika dunia hii yenye changamoto nyingi. Amesema

“Kwa Afrika, haya yanapaswa kutukumbusha mahali tulipo katika mwelekeo wa dunia ya leo, kwa sababu tumekuwa na watu wengi wanaotushirikisha mawazo yenye msingi na kutufundisha namna tunavyopaswa kufanya kazi pamoja na jinsi tunavyopaswa kutekeleza mambo hayo.     

Hata hivyo, nasi hatupaswi kubaki palepale, bali tunapaswa kujifunza kutokana na hali hiyo. Unaona sababu zilizoifanya Afrika kurudi nyuma miaka ya nyuma. Tunapaswa kuelewa ni kwa nini tunakosa mafanikio ilhali tuna kila kitu kinachohitajika.”

Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni ya  Jeune Afrique Amir Ben Yahmed na ambayo huandaa mkutano  wa Africa CEO Forum, amesema kuwa katika kipindi cha miaka 15,  umepiga hatua kubwa.

“Kwanza kabisa, sekta binafsi  zimepata maendeleo ya kuaminika katika kipindi cha miaka 15..Uwekezaji wa kimataifa unahitajika, lakini jambo muhimu zaidi ni namna unavyofanywa katika kugawana thamani ya soko letu.  Kwa mfano, kampuni nyingi za kimataifa ziko hapa na  zimeanza kufikiria jinsi ya kusajili uwekezaji wao.”

Naye Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu amesema kuwa mambo yanayosemwa kwa maneno inatakiwa yawekwe  kwa vitendo: “Tunahitaji kuweka fedha kwenye vitendo badala ya kuishia kuyazungumzia tu, na kujenga ushirikiano unaochochea maendeleo ya biashara barani Afrika, siyo mambo ya kubaki kwenye maneno au maandishi pekee.”

Mkurugenzi Mkuu wa RDB, Jean-Guy Afrika, amesema kuwa fursa iliyopo katika idadi kubwa ya watu wa Afrika haipaswi kupuuzwa. Alieleza kuwa fursa hiyo inapaswa kuambatana na juhudi za kuitumia kwa maendeleo katika sekta mbalimbali kama biashara na uwekezaji. Amesema kuwa sekta binafsi inapaswa kushiriki kikamilifu kwa kufanya uwekezaji unaochochea maendeleo.

Akitoa mfano wa Rwanda, amesema kwamba nchi hiyo imefungua milango kwa wawekezaji na kufanya uwekezaji katika sekta mbalimbali kama utalii, teknolojia na nyinginezo, huku pia ikiweka mageuzi yanayowezesha wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini humo.

Marais walioshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria, Brice Clotaire Oligui Nguema wa Gabon, Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania, Mamadi Doumbouya wa Guinea na Daniel Chapo wa Msumbiji.

Africa CEO Forum ni kongamano kubwa la biashara na uwekezaji linalowakutanisha viongozi wakuu wa makampuni, marais wa nchi, wawekezaji na wanasheria kutoka Afrika na duniani kote.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *