EADB yatangaza Mfuko wa Dola Milioni 13 kwa Vijana na Wanawake
Na Christopher Karenzi
chriskarenzi@gmail.com
Kampala, Uganda Jumatatu, Mei 11, 2026, Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) imetangaza kuanzishwa kwa mfuko wa dola milioni 13 za Marekani kwa ajili ya kusaidia biashara zinazoongozwa na vijana na wanawake katika ukanda wa Afrika Mashariki, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha jumuishi katika eneo hilo.
Mfuko huo ulitangazwa wakati wa kikao cha Baraza la Uongozi la Benki hiyo kilichofanyika Kampala, na umejengwa katika Mpango Mkakati wa EADB wa mwaka 2024–2028 pamoja na dhamira ya benki ya kuendeleza maendeleo endelevu na shirikishi ya kijamii na kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wake.
Tangazo hilo limekuja wakati Benki hiyo ikiripoti matokeo mazuri ya kifedha, baada ya kurekodi ongezeko la asilimia 51 katika faida. Faida kabla ya kodi ilifikia dola milioni 16.93 za Marekani kwa mwaka ulioishia Desemba 2025, ikilinganishwa na dola milioni 11.20 katika mwaka wa fedha uliotangulia.
EADB pia ilirekodi ukuaji mkubwa katika shughuli zake za utoaji mikopo, ambapo kiwango cha fedha zilizotolewa kama mikopo kiliongezeka kwa asilimia 140, huku thamani ya mikopo iliyokuwa haijalipwa mwishoni mwa mwaka ikiongezeka kwa asilimia 52. Hali hiyo inaonyesha kuimarika kwa utendaji wa jalada la mikopo pamoja na ufanisi wa shughuli za benki hiyo.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Baraza la Uongozi, Mheshimiwa Matia Kasaija, ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwezo mkubwa wa benki katika kukusanya mitaji na kutumia mbinu bunifu za ufadhili katika sekta mbalimbali. Amesema :“Mafanikio haya makubwa ni ushahidi wa uwezo ulioimarishwa wa EADB katika kuhamasisha rasilimali na kutumia suluhisho bunifu za kifedha.
Katika mwaka uliopita, tuliwezesha miradi mbalimbali katika sekta muhimu ndani ya nchi wanachama wetu. Tunaendelea kujizatiti kutekeleza Mpango wetu wa Mkakati wa miaka mitano huku tukipanua jalada letu la uwekezaji na kuongeza mchango wetu wa maendeleo katika ukanda huu,” amesema.

Kikao hicho cha Baraza kilihudhuriwa na Waziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la EADB, Mheshimiwa Matia Kasaija; Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi wa Rwanda na mjumbe wa Baraza la Uongozi la EADB, Mheshimiwa Yusuf Murangwa; Waziri wa Hazina ya Taifa na Mipango ya Uchumi wa Kenya pamoja na mjumbe wa Baraza la Uongozi la EADB, Mheshimiwa FCPA John Mbadi Ng’ongo EGH; Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mjumbe wa Baraza la Uongozi la EADB, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar; pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya EADB. Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ilianzishwa mwaka 1967 chini ya mkataba wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo.

Dhamira yake ilikuwa kutoa msaada wa kifedha na huduma zinazohusiana kwa taasisi na biashara katika nchi wanachama ambazo shughuli zake zilitarajiwa kuchangia maendeleo chanya ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo. Benki hiyo ilianzishwa upya mwaka 1980 chini ya Hati Mpya ya Makubaliano (Charter).
Kupitia Hati hiyo, jukumu na mamlaka ya Benki yalifanyiwa mapitio na wigo wa shughuli zake kupanuliwa ili kujumuisha huduma mbalimbali za kifedha katika nchi wanachama, kwa lengo kuu la kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na mshikamano wa kikanda.
Kwa sasa, EADB inamilikiwa na nchi nne wanachama ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda, pamoja na taasisi nyingine za maendeleo na kifedha za kibiashara. Kwa kuwa ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ushirikiano wake na taasisi za EAC umeiwezesha kuwa na nafasi muhimu ya kuchochea mchakato wa ushirikiano wa kikanda kupitia utoaji wa fedha za maendeleo.
