Rwanda yaunganisha miundombinu yake ya kusafirisha umeme na nchi jirani zake
Na Christopher Karenzi
Jijini Kigali nchini Rwanda, kunafanyika maonyesho pamoja na mkutano wa siku tatu unaohusu ubunifu mpya katika kuendeleza sekta ya nishati barani Afrika, ujulikanao kama (Africa Energy Expo Summit). Rwanda ni miongoni mwa wanachama wa umoja wa Eastern Africa Power Pool, unaojumuisha nchi 13 za Ukanda wa Afrika Mashariki, zinazoshirikiana katika masuala ya nishati)).
Kupitia umoja huo, nchi wanachama zinapanga kuunganisha mitandao yake ya kusafirisha umeme, ili kurahisisha kubadilishana nishati kulingana na mahitaji ya kila nchi, pamoja na kuuziana umeme.

Mkutano huo wa kimataifa umewaleta kwa pamoja watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wakiwemo mawaziri , viongozi wa makampuni ya usambazaji wa umeme, viongozi wa mashirika pamoja na wafanyabiashara.
Milton Mkhweli ni Mtaalamu wa Maendeleo ya Biashara kutoka nchini Afrika ya kusini ni miongoni mwa walioleta vifaa vya nishati kwenye maonyesho hapa Kigali. Alikuwa na haya ya kusema: “Lengo la Afrika ni kupata wataalamu huru na wenye uweledi watakaowezesha kuimarika kwa mifumo ya nishati endelevu barani Afrika. Wataalamu wanaoweza kuziba mapungufu ya muda kwenye masuala ya kitaalamu barani Afrika pale inapohitajika kujaza pengo la utaalamu.”Tumejenga hifadhi data yenye wataalamu elfu tisa. Aidha, tunafanya kazi na wateja mbalimbali wanaohitaji huduma za kitaalamu katika maeneo tofauti barani.”
Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, Dkt. Jimmy Gasore, amesema kuwa Rwanda inaendelea kushirikiana kwa karibu na nchi za eneo hilo katika kugawana miundombinu ya umeme. Amesema ‘’Tunatarajia kuwa mkutano huu utasaidia kuwaleta pamoja wadau wote ili kuongeza nguvu za pamoja na kuhakikisha utoaji wa umeme wa kutosha kwa Waafrika wanaouhitaji.
‘’ Kwa upande mwingine, wananchi wa Rwanda wanaotembelea ukumbi wa Convention Centre wanaweza kuona vifaa vya kisasa, hususan teknolojia za kutumia nishati ya jua. Haya yanaonekana kuwa fursa mpya na muhimu kwa nchi’’ Waziri Gasore ameongeza.

Dr Gasore amebainisha kuwa mtandao mpya wa kusafirisha umeme kati ya Rwanda na Burundi kupitia Wilaya ya Huye tayari umekamilika.
Kulingana na waandalizi wa mkutano, tangu jana tukio hilo limepokea zaidi ya wataalamu wa sekta ya nishati elfu moja kutoka zaidi ya nchi 40, ambapo mikutano ya ana kwa ana imerahisisha kupatikana kwa mikataba mipya na ushirikiano pia.
Aidha, Rwanda imeunganisha miundombinu yake ya kusafirisha umeme na nchi jirani za Uganda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na Burundi katika maeneo matatu tofauti.
Katika kituo cha Rusizi II, nchi tatu Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinashirikiana kupata umeme wa jumla ya megawati 36, ambapo kila nchi hupokea megawati 12. Mkutano huu utatamatika kesho alhamisi tarehe 27 Novemba 2025.
