Waziri Nduhungirehe: Wanajeshi hawawezi kuendelea kufanya kazi huku wakiwekewa vikwazo na shinikizo la mara kwa mara.

Share Now

Christopher Karenzi

Kufuatia vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) na majenerali wanne mwanzoni mwa mwezi huu, vikiwashutumu kwa kusaidia kundi la waasi la M23 katika vita vinavyoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuna wasiwasi kuhusu iwapo RDF  pamoja na washirika wake,  wataweza kuendelea na baadhi ya shughuli za kurejesha usalama nchini Mozambique kutokana na vizuizi vinavyotokana na vikwazo hivyo vilivyowekwa na Wizara ya Fedha ya Marekani.

Olivier Nduhungirehe amesema kuwa majeshi ya Rwanda hayawezi kuendelea kutekeleza jukumu lao huku yakikosolewa kila siku na kuwekewa vikwazo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Nduhungirehe, alieleza kuwa iwapo msaada uliokuwa unatolewa na Umoja wa Ulaya katika operesheni za kupambana na ugaidi nchini Msumbiji utasitishwa, basi majeshi ya Rwanda yaliyoko katika nchi hiyo yataondoka mara moja, na nafasi yao ichukuliwe na majeshi kutoka nchi nyingine.

Waziri Nduhungirehe, ameonya kuwa Rwanda “itaondoa wanajeshi wake” katika operesheni ya kupambana na ugaidi katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji amebaini kuwa  shughuli za kiuchumi zimerejea eneo hilo. Amesema: “Tumefanya kazi kubwa kiasi kwamba raia wamerudi majumbani mwao, wanafunzi wamerudi shuleni, shughuli za kiuchumi zimeanza tena, uwekezaji mkubwa katika sekta ya gesi umeanza upya, na kampuni zimeanza kufanya kazi tena. Haya yote yamewezekana kupitia ushirikiano kati ya majeshi ya Rwanda na yale ya Msumbiji.”

Waziri Nduhungirehe amebaini kuwa jumuiya ya kimataifa inaendelea kuyawekea majeshi yaliyo katika operesheni hiyo chini ya shinikizo, hali ambayo anasema inaweza kukwamisha juhudi za kurejesha amani na usalama: “Tunakumbusha kwamba Rwanda pia imetoa mchango mkubwa, ikitoa fedha nyingi zaidi ya mara kumi ya zile tunazopokea kutoka Umoja wa Ulaya na pia tumepoteza wanajeshi wetu waliouawa vitani ili kuleta utulivu katika eneo hilo. Kwa hiyo, wanajeshi hao hawawezi kuendelea kufanya kazi hiyo huku wakikosolewa kila mara, kuwekewa vikwazo na shinikizo la mara kwa mara.

Kwa upande wetu, ushirikiano kati ya Msumbiji na Rwanda unaendelea. Ni wazi kuwa ushirikiano huo unaweza kuathiriwa na mwenendo wa nchi zinazotuwekea vikwazo.”

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na DRC na nchi za Magharibi, wanaishutumu Rwanda kwa kusaidia kundi la M23 linalopambana na serikali ya DRC, kwa kulipatia wanajeshi, vifaa na msaada wa kimkakati

Aidha,Serikali ya Rwanda inakanusha kuisaidia kundi la M23, ikisema kuwa imechukua “hatua za kujilinda”.  Kufuatia vikwazo vya Marekani vya mwezi huu, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliwaambia wanadiplomasia mjini Kigali  kuwa, kutokana na historia ya Rwanda  na mahali ilipo, bado inahitaji mipaka ya ulinzi ili kufikia lengo hilo pekee.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *