Stephen Constantine ateuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi).
Na Karenzi Christopher
Rais wa Shirikisho la soka ncjini Rwanda FERWAFA, Shema Ngoga Fabrice, amesema kuwa moja ya sababu kuu zilizowafanya kumpa kazi Constantine ni kwamba alikuwa tayari kuanza kazi mara moja na pia alikuwa na hamu ya kurejea nchini hapa.
Tarehe 12 Machi 2026, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda lilitangaza rasmi kuwa kocha huyu mwenye asili ya Cyprus na Uingereza ndiye atakayeinoa timu ya taifa ya Rwanda. Constantine alichaguliwa baada ya FERWAFA kutoa tangazo la kutafuta mbadala wa Adel Amrouche, ambaye walitengana naye tarehe 14 Januari 2026 baada ya mwaka mmoja kazini.
Jumla ya makocha 688 waliwasilisha maombi yao wakionekana kukidhi vigezo. Kisha kulifanyika mchakato wa uchujaji kulingana na vyeti, uzoefu wa kufundisha timu za taifa, na ushiriki wao katika mashindano makubwa kama Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia.

Hata hivyo, baada ya kutangazwa kwake, baadhi ya watu hawakuridhishwa na uteuzi wake wakisema kuwa hakutimiza baadhi ya vigezo vilivyotangazwa.
Ngoga alisisitiza kuwa kocha aliyetakiwa alipaswa kuwa na rekodi ya mafanikio, hasa kuifikisha timu kwenye mashindano ya bara. Alisema:
“Lazima awe na historia ya kuiwezesha timu kufuzu michuano ya bara akiwa anaifundisha.” Vigezo vingine vilijumuisha uwezo wa kuipandisha timu katika viwango vya FIFA na kuwa tayari kuanza kazi mara moja. Aliongeza: “Mtu ambaye anaweza kusaidia timu kupanda katika viwango vya FIFA na kuanza kazi haraka.”
Rwanda iliwahi kupata nafasi nzuri katika viwango vya FIFA ilipokuwa ikifundishwa na Constantine, ambapo ilifikia nafasi ya 64 duniani.
Kwa upande wake, Constantine alisema amerudi kukamilisha kazi aliyokuwa ameiacha. Amesema: “Nimerudi kumalizia kazi niliyoiacha miaka 11 iliyopita. Hatukufuzu AFCON kwa sababu tulishtakiwa kwa kutumia mchezaji mwenye utambulisho zaidi ya mmoja, lakini nina furaha kurejea hapa.”
Ngoga pia ameeleza kuwa kati ya makocha 688 walioomba kazi, 20 walichaguliwa kwa usajili, wakabaki 5, na hatimaye 3 bora, ambapo Constantine ndiye aliyechaguliwa kuinoa Amavubi kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Rais wa Ferwafa Shema Ngoga Fabrice
