Serikali ya Repubulika ya DRC yasita kuwapokea wanajeshi 5000 waliotekwa na AFC/M23

Share Now

Na Christopher Karenzi

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, imeonyesha kusita kuwapokea wanajeshi 5000 waliotekwa na muungano wa AFC/M23, ikieleza hofu kuwa wanaweza kuisaliti.

Muungano wa AFC/M23 unashikilia maelfu ya wanajeshi wa serikali, wengi wao wakitekwa wakati wa mapigano ya kuuteka mji wa Goma na maeneo ya mpakani yaliyotokea mwishoni mwa Januari 2025.

Tarehe 8 Machi 2026, AFC/M23 ilitangaza kuwa itawakabidhi wanajeshi 5000 kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ili iwapeleke  mjini Kinshasa.

Muungano huo unaleza kuwa uamuzi wa kuwaachilia wanajeshi hao, waliokuwa wamehifadhiwa katika kambi ya kijeshi ya Rumangabo, ulikuwa wa kusaidia kufanikisha mazungumzo ya amani kati yao na serikali ya DRC, ili kupatikana amani ya kudumu.

Mnamo tarehe 8 Aprili 2026, Redio ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI) iliripoti kuwa ICRC iko tayari kuwasafirisha wanajeshi hao hadi Kinshasa, lakini serikali ya DRC bado haijakubali kuwapokea kutokana na hofu kwamba huenda miongoni mwao kuna “maadui”.

Redio hiyo ilieleza kuwa AFC/M23 inaendelea kuweka shinikizo kwa serikali ya DRC ili iwapokee wanajeshi hao, lakini mtu wa karibu na Rais Félix Tshisekedi alishangaa sababu ya kulazimishwa kufanya hivyo. Alisema: “Kwa nini wanatulazimisha? Je, wanafanya hivyo kwa hiari yao au kuna sababu nyingine iliyojificha nyuma yake?”

Tarehe 20 Februari 2026, kiongozi wa AFC/M23, Corneille Nangaa Yobeluo, alitangaza kuwa muungano huo utaachilia wanajeshi 230 waliotekwa katika mji wa Goma, ingawa haijajulikana kama walipelekwa Kinshasa na ICRC.

Mnamo Aprili 2025, wanajeshi na polisi 1359 wa DRC waliokuwa wamekimbilia katika kambi za vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO) karibu na Goma, walipelekwa Kinshasa baada ya mazungumzo kati ya ICRC na AFC/M23.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *