Karenzi
Rwanda yatuma wanajeshi Jamaica kusaidia ukarabati wa miundombinu
Na Christopher Karenzi
chriskarenzi@gmail.com
Jeshi la Rwanda (RDF) limetuma kikosi cha Jeshi la ujenzi nchini Jamaica, kwa lengo la kusaidia nchi hiyo kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na majanga ya asili yaliyosababishwa na kimbunga kilichoitwa Hurricane Melissa, ambacho kilikumba Jamaica mwishoni mwa mwaka jana na kuacha uharibifu mkubwa.
Wanajeshi hao wametumwa kufuatia makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Rwanda na Jamaica, yanayolenga kutoa msaada katika ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na majanga ya asili.
Kabla ya kuondoka Rwanda tarehe 14 Januari 2026, Kamanda wa Divisheni inayohusika na uendeshaji wa magari ya kivita ndani ya RDF, Brigedia Jenerali Faustin Tinka, aliyemwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, aliwakumbusha wanajeshi hao kutumia kikamilifu maarifa, taaluma na ujuzi wao ili kutekeleza vyema jukumu walilopewa na uongozi wa RDF.

Kiongozi huyo pia aliwahimiza kufanya kazi kwa namna ambayo itawafanya wananchi watakaonufaika na msaada huo kuthamini mchango wao, huku wakijitahidi kuzingatia maadili ya RDF, ikiwemo nidhamu na adabu, kama msingi wa utendaji wa Jeshi la Rwanda.

Kamanda wa Divisheni ya uendeshaji wa magari ya kivita ndani ya RDF, Brigedia Jenerali Faustin Tinka, amewataka wanajeshi kuzingatia maadili ya RDF.
Alisema: “Ni maadili haya ndiyo yaliyowafanya mpate jukumu hili.” Aliwakumbusha kuwa wanapaswa kuendelea kuyazingatia maadili ya RDF wakati wote.
Wanajeshi hao wamehimizwa kutumia maarifa, taaluma na ujuzi wao ili kukamilisha vyema jukumu walilopewa na uongozi wa RDF
Kimbunga Hurricane Melissa kilikumba visiwa vya Karibea mwishoni mwa Oktoba 2025, na kusababisha athari kubwa nchini Jamaica, hali iliyopelekea kuanzishwa kwa operesheni kubwa za uokoaji wakati nchi hiyo ikiendelea na juhudi za kujijenga upya.
