Balozi Bazivamo achukua mikoba ya  Gasamagera kama Katibu Mkuu wa RPF

Share Now

Na Brightafica.rw

Mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe, Christophe Bazivamo, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala cha Rwanda Patriotic Front (RPF-Inkotanyi) baada ya kuthibitishwa na mkutano mkuu wa chama uliofanyika Ijumaa, tarehe 19 Desemba.

Bazivamo amechukua nafasi ya Wellars Gasamagera, naye pia akiwa mwanadiplomasia wa zamani, ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu mwaka 2023.

Uteuzi huo umetangazwa katika Mkutano wa 17 wa RPF uliofanyika katika makao makuu ya chama eneo la Rusororo, ambapo wajumbe pia wamepitisha mageuzi ya muundo wa uongozi wa chama. Miongoni mwa maamuzi muhimu ya mageuzi hayo ni kuanzishwa kwa Baraza la Wazee kama mojawapo ya vyombo vya chama.

Balozi Bazivamo Christophe (katikati akiwa amesimama), kateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha RPF Inkotanyi

Mkutano huo pia uliidhinisha wajumbe wapya wa Kamati Tendaji, akiwemo Consolée Uwimana kama Makamu Mwenyekiti wa Kwanza, Marie Solange Kayisire kama Makamu Mwenyekiti wa Pili, na Stephen Gasana Karasanyi kama Naibu Katibu Mkuu.

Bi Uwimana Consolée, Waziri wa Jinsia na Masuala ya Familia, alikuwa tayari akihudumu nafasi kama hiyo ndani ya chama. Consolée Uwimana ameteuliwa tena kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa RPF-Inkotanyi.

Bazivamo ni kada mwandamizi wa RPF mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi. Hivi karibuni alikuwa Makamu Mwenyekiti wa chama, wadhifa alioutumikia kuanzia mwaka 2002 hadi 2023.

Balozi Bazivamo alihuumu katika utumishi wa umma, aliwahi kuwa mjumbe wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Waziri wa Serikali za Mitaa, Maendeleo ya Jamii, Habari na Masuala ya Kijamii, Waziri wa Usalama wa Ndani, pamoja na Waziri wa Ardhi, Mazingira, Misitu, Maji na Madini, miongoni mwa nyadhifa nyingine. Aidha, ni mwanadiplomasia na kwa sasa anahudumu kama Balozi Mkuu wa Rwanda nchini Nigeria.

Marie Solange Kayisire ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Pili

Stephen Gasana Karasanyi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *