M23 Yapinga Wito wa Ufaransa wa kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa Goma

Share Now

Na Christopher Karenzi

Muungano wa ”Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), kinachodhibiti maeneo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kimepinga tamko la hivi karibuni la Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, aliyetoa wito wa kufunguliwa tena uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Goma.

M23 imesema uamuzi huo “haumbatani na hali halisi ya mambo yanayoendelea Goma, na umechukuliwa bila kushauriana na pande husika.”

Katika taarifa iliyotolewa na Corneille Nangaa, Kiongozi wa muungano wa AFC–M23, kundi hilo lilionyesha mshangao kwamba tangazo hilo lilitolewa mjini Paris, wakati wa mkutano wa kimataifa uliojadili misaada ya kibinadamu kwa eneo la maziwa Makuu, bila kufanyika kwa mashauriano au tathmini ya kina ya hali ya usalama huko Kivu.

Nangaa amesema: “Uamuzi huu umechukuliwa kwa pupa, hauendani na ukweli wa mambo, na haukuzingatia maoni ya AFC/M23.”

Rais Macron alitangaza mpango wa kufunguliwa kwa uwanja wa ndege wa Goma  Alhamisi, Oktoba 30, wakati wa mkutano ulioitwa “International Conference for Peace and Prosperity in the Great Lakes Region” uliofanyika Paris, ambapo aliketi pamoja na Rais wa DR Kongo Félix Tshisekedi, kiongozi wa Togo, na wajumbe kutoka nchi mbalimbali.

Macron alisema uwanja wa ndege wa Goma utafunguliwa tena “katika wiki chache zijazo” ili kurahisisha safari za ndege za misaada na kufikisha huduma kwa wakazi wa mashariki mwa Kongo wanaoteseka kutokana na vita.

Alisisitiza kwamba hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za “kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na kuimarisha shughuli za kibinadamu.”Akasema: “Kufunguliwa tena kwa uwanja wa Goma kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ni hatua muhimu katika kurejesha matumaini na maisha kwa wananchi wa mashariki mwa Kongo. Ufaransa, pamoja na washirika wake, watahakikisha misaada inafika mahali panapohitajika.”

Macron pia alifichua kwamba jumuiya ya kimataifa tayari imekusanya euro bilioni 1.5 (€1.5 billion) kusaidia miradi ya misaada na ujenzi wa kiuchumi katika eneo la Maziwa Makuu, ikiwemo DRC, Rwanda, Burundi, na Uganda. Alizitaka pande zote “kusitisha mapigano na kuruhusu misaada kufika kwa walioathirika.”

Rais wa Togo Faure Gnassingbé

Kwa upande wake, Nangaa alisema tamko la Macron  halina msingi kwani wakati anazungumzia misaada, “jeshi la serikali ya Kongo na washirika wake wanaendelea kushambulia raia, kuvunja viwanda, madaraja, na hata kulenga ndege za misaada.”

Amesema: “Ni unafiki kusema uwanja wa ndege utatumika kwa misaada, ilhali wahudumu wa misaada na raia wanaolengwa na misaada hiyo wanashambuliwa kila siku.”

AFC–M23 pia ililaani kile ilichokiita “kuvuruga uchumi wa raia wa Goma,” ikisema benki zimefungwa na wananchi hawawezi kutoa fedha zao, jambo lililoathiri vibaya maisha ya kiraia.

Kundi hilo lilitaja changamoto kadhaa zinazoathiri mchakato wa kurejesha amani, ikiwemo mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yanayolenga raia, na mashambulizi dhidi ya ndege za misaada katika maeneo ya Walikale na Minembwe. Pia lilishutumu serikali ya Kinshasa kwa “kufunga anga” katika maeneo yanayodhibitiwa na M23 ili kurahisisha mashambulizi ya kijeshi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa pamoja na Rais wa DRC Félix Tshisekedi

Nangaa alisisitiza kuwa maeneo yanayodhibitiwa na AFC–M23 yana amani na utulivu, huku akituhumu Kinshasa kwa kuendelea “kuchochea vurugu.”

Alishutumu pia makundi yanayojinufaisha kupitia misaada ya kibinadamu, akisema wanatumia mateso ya wakimbizi kwa maslahi ya kisiasa na kifedha, akitaka Ufaransa “kutojenga sera zake juu ya watu wanaotumia mateso ya wengine kujitajirisha.”

Amesema: “Ufaransa haipaswi kuwaunga mkono wanaotumia mateso ya watu kwa faida binafsi, bali ifaidi miradi itakayolinda kwa amani ya kudumu.”

Taarifa hiyo ilisisitiza kwamba AFC–M23 imejizatiti kuendeleza njia ya amani kupitia mazungumzo, kwa mujibu wa mipango kama ile ya mazungumzo ya Doha, na ikatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za amani za kweli si zile zinazochochea vita vipya.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *