Timu ya Sudan yawasili Kigali,kujiandaa ligi ya RPL

Share Now

Na Christopher Karenzi

Klabu ya Al Hilal Omdurman kutoka Sudan, ambayo inatarajia kushiriki katika Ligi Kuu ya Rwanda msimu wa 2025/2026, imewasili jijini Kigali na kupokelewa kwa furaha kubwa na raia wa Sudan wanaoishi nchini Rwanda.

Timu hiyo iliwasili katikaUwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali ulioko Kanombe alfajiri ya Ijumaa, Oktoba 31, 2025, baada ya kuondoka nchini Libya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Benina siku ya Alhamisi asubuhi.

Mara tu baada ya kuwasili Kigali, Al Hilal Omdurman ilipokelewa kwa shangwe na raia wa Sudan wanaoishi Rwanda, wakiongozwa na Balozi wa Sudan nchini Rwanda, Khalid Musa Dafalla.

Baada ya mapokezi hayo, timu hiyo ilielekea Zaria Court Hotelkwa ajili ya malazi ya muda kabla ya kupata makazi ya kudumu. Aidha, timu hiyo itakuwa ikichezea mechi zake za Ligi Kuu ya Rwanda na zile za CAF Champions Leaguekatika Uwanja wa Amahoro.

Wakati huo huo, klabu nyingine kutoka Sudan, Al-Merrikh, nayo imeomba kushiriki katika Ligi Kuu ya Rwanda na imetangaza kuwa itawasili nchini Rwanda tarehe 4 Novemba 2025, ikitokea Libya.

Timu hizi za Sudan zimeomba kushiriki Rwanda Premier League baada ya ligi yao ya ndani kusitishwa kutokana na hali ya ukosefu wa usalama nchini mwao.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *