Vijana wengi wenye vipaji hukumbana na changamato kwa kupata ajira zenye tija
Na Christopher Karenzi
Jackal TECH Ltd ni kampuni changa ya teknolojia (startup) ya Rwanda iliyoanzishwa mwaka 2019 na kufanyiwa mabadiliko ya chapa (rebranding) mwaka 2021 ili kujikita kama kampuni ya teknolojia inayolenga kuendeleza suluhisho bunifu za kidijitali.
Ignace Kwizera ni Mkurugenzi Mtendaji (CEO ) wa Jackal TECH Ltd na Mwanzilishi Mwenza wa Jocotech Limited nchini Rwanda, akiongea na Brightafrica, amesema: ‘’Tangu kuanzishwa kwake, kampuni imekuwa ikifanya kazi katika sekta tatu kuu: Teknolojia ya Elimu (EdTech), Teknolojia ya Afya (HealthTech), na Teknolojia ya Biashara ya Rejareja (RetailTech)’’.
Kwa miaka kadhaa, Jocotech imekuwa ikiunda na kuendeleza suluhisho mbalimbali za kiteknolojia zinazolenga kutatua changamoto katika sekta hizi. Hata hivyo, kuanzia mwaka 2024, kampuni ilifanya uamuzi wa kimkakati wa kuelekeza nguvu zake zaidi katika Teknolojia ya Elimu (EdTech). Kwizere amesema: ‘’Kupitia mipango yake ya EdTech, Jocotech imejizatiti kuwapatia wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana wataalamu uzoefu wa vitendo unaowasaidia kuziba pengo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira la kimataifa’’.

Ignace Kwizera ni Mkurugenzi Mtendaji (CEO)
Kampuni ilibaini changamoto kubwa kwamba wahitimu wengi wa vyuo vikuu humaliza masomo yao bila kuwa na ujuzi wa vitendo na uzoefu unaohitajika na waajiri pamoja na wajasiriamali katika uchumi wa kisasa wenye ushindani mkubwa.
Kutokana na hali hiyo, vijana wengi wenye vipaji hukumbana na changamato kwa kupata ajira zenye tija, kuanzisha biashara zao wenyewe, au kuchangia ipasavyo maendeleo ya jamii zao. Ili kukabiliana na changamoto hii, Jocotech imebuni programu na suluhisho mbalimbali zinazowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa kazi katika mazingira halisi, ujuzi unaohitajika na sekta mbalimbali, pamoja na fursa za kushiriki katika masoko ya kimataifa.
Tangu mwaka 2024, dhamira ya kampuni imekuwa ni kubadilisha mfumo wa elimu kwa kuunganisha maarifa ya darasani na matumizi ya vitendo, hivyo kuwawezesha wanafunzi kuwa wataalamu walio tayari kwa ajira, wajasiriamali wabunifu, na wachangiaji muhimu katika maendeleo endelevu ya kiuchumi.
