Rwanda yajua kundi ililopangwa katika FIFA Series itakayofanyika Kigali

Share Now

Na Christopher Karenzi

Timu ya Taifa ya Rwanda “Amavubi” imepangwa katika Kundi A pamoja na Estonia, Grenada na Kenya katika mashindano yatakayozikutanisha timu za taifa kutoka mabara mbalimbali, yaliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), yajulikanayo kama FIFA Series. Mashindano hayo yatafanyika Kigali kuanzia tarehe 23 hadi 31 Machi 2026.

Droo ya upangaji wa timu nane zitakazoshiriki mashindano hayo, zilizogawanywa katika makundi mawili, ilifanyika Jumatatu tarehe 19 Januari 2026.

Rwanda, kama mwenyeji wa mashindano, imepangwa katika Kundi A pamoja na Estonia, Grenada na Kenya, huku Kundi B likiwa na timu za Aruba, Liechtenstein, Macau na Tanzania.

Mechi hizi za kirafiki zitazikutanisha timu za taifa za wanaume kutoka mabara tofauti. Mashindano haya ni sehemu ya mpango wa FIFA wa miaka 2023–2027, wenye lengo la kutoa fursa kwa timu ambazo kwa kawaida hazipati mechi nyingi za kirafiki au hazipati nafasi ya kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.

Hadi sasa, timu ya taifa ya Rwanda haina kocha mkuu, baada ya kumfuta kazi kocha raia wa Algeria Adel Amrouche, aliyekuwa Kocha Mkuu, kwa sababu ya kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wake wa ajira.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *