Rais Museveni: ‘’Raia wa Uganda hawapaswi kumsikiliza Kyagulanyi anayewahamasisha kuingia katika maandamano’’
Na Christopher Karenzi
Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amewaonya raia wa Uganda kutojihusisha na kile alichokiita ushawishi wa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, ambaye hivi karibuni alisema kuwa raia wanaweza kuwazidi nguvu vyombo vya usalama kwa sababu wako wengi kwa idadi.
Museveni alirejelea kauli za Kyagulanyi, ambaye wanatarajiwa kushindana naye katika uchaguzi wa urais, usiku wa Jumatano tarehe 17 Desemba 2025, akiwa katika eneo la Kisozi nyumbani kwake. Mazungumzo hayo yalirushwa kupitiaRuninga ya Taifa ya Uganda (UBC) pamoja na redio mbalimbali nchini humo.
Rais Museveni alisema kuwa raia wa Uganda hawapaswi kumsikiliza Kyagulanyi anayewahamasisha kuingia katika maandamano. Alisema
“Nimesikia Kyagulanyi akisema kuwa askari ni wachache na waandamanaji ni wengi. Kwa kweli msimsikilize Kyagulanyi, msifuate anachosema kwa sababu hakitazami mbele. Kila askari ana risasi 120, hivyo jihesabieni hilo. Kabla ya kusema waandamanaji ni wengi, anzeni kuhesabu idadi ya askari. Nendeni mkapige kura, hakuna atakayevuruga Uganda, na yeyote atakayethubutu kufanya hivyo atajuta.”
Museveni alitoa kauli hizo wakati ambapo katika kampeni za Kyagulanyi kumekuwa na vurugu na hali inayofanana na maandamano katika siku za hivi karibuni, hali ambayo imeilazimu serikali kutumia vyombo vya usalama kurejesha utulivu.
Uchaguzi wa Rais wa Uganda unatarajiwa kufanyika tarehe 15 Januari 2026. Rais Museveni, ambaye ameitawala Uganda kwa karibu miaka 40, ndiye anayetajwa kuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo.

Rais Yoweri Museveni
