RAIS KAGAME: Afrika bado yahitaji uwekezaji wa kweli katika sekta ya anga

Share Now

Mwandishi Christopher Karenzi

Kigali – Rais Paul Kagame amesema kuwa Bara la Afrika bado lina safari ndefu ya kupiga hatua katika sekta ya anga, akisisitiza kuwa kunahitajika uwekezaji wa kweli na wa kudumu ili bara hili liweze kunufaika ipasavyo na fursa kubwa zilizopo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tisa wa Aviation Africa Summit and Exhibition 2025 ulioanza jana katika Kigali Convention Center, Rais Kagame alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na kuwekeza katika teknolojia za kisasa, akitolea mfano drones mpya zinazobeba abiria ambazo zimezinduliwa kwa mara ya kwanza nchini Rwanda.

“Rwanda inajivunia kuwa sehemu ya historia hii. Tuko tayari kushirikiana na washirika wote katika kukuza teknolojia hii mpya ya anga,” alisema Rais Kagame. Drones hizo, zijulikanazo kama eVTOL, zimetengenezwa na kampuni ya Kichina EHang na zinatumia umeme kwa asilimia 100.

Rais Kagame pia alisifu mchango wa Zipline Rwanda, kampuni ambayo kwa karibu miaka kumi sasa imekuwa ikisafirisha damu katika maeneo mbalimbali ya nchi, akisema kuwa imeokoa maisha ya watu wengi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Alan Peaford, aliushukuru zaidi uongozi wa Rwanda kwa kuandaa kongamano hilo, akieleza kuwa limevutia wageni wa hadhi kubwa wakiwemo mawaziri tisa kutoka nchi tofauti na wakuu wa mashirika ya ndege za kiraia wapatao 30. “Ni ushiriki wa kiwango cha juu ambacho hakijawahi kushuhudiwa,” alisema.

Peaford aliwakumbusha washiriki kuwa changamoto kuu zinazokwamisha sekta ya anga barani Afrika ni ukosefu wa uratibu baina ya nchi, mifumo isiyo na ufanisi na ucheleweshaji katika kupokea miongozo ya kimataifa. “Tusiposhirikiana, Afrika itaendelea kurudi nyuma,” alionya.

Aidha, alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi siyo tu katika urubani, bali pia kupitia mafunzo na fursa zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta hii.

Mkutano huu wa siku mbili umewakutanisha waoneshaji 120 na kampuni zaidi ya 90 za ndege, ambapo mjadala mkubwa unahusu mikakati ya kuunganisha safari za ndege barani Afrika, kuimarisha miundombinu, sheria na kukuza rasilimali watu.

Kwa kauli mbiu isemayo: “Kushirikiana katika kufungua fursa za maendeleo ya Afrika: Jinsi gani Afrika inaweza kujenga sekta ya anga endelevu?”, kongamano hili linaweka Kigali kwenye ramani kama kitovu cha mazungumzo ya mustakabali wa anga barani Afrika.

Brightafrica


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *