Rais Kagame: Kukutana na DRC jijini Washington ni hatua muhimu
Na Christopher Karenzi
chriskarenzi@gmail.com
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amesema kuwa kundi la kigaidi la FDLR bado ni tishio kubwa kwa Rwanda na eneo la Maziwa makuu na kwamba hata kundi dogo la wapiganaji linaweza kusababisha madhara makubwa. Ameyesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari alhamis tarehe 27 Novemba 2025 katika Ikulu ya Rais jijini Kigali.
Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kuwa Serikali ya DRC inashirikiana na FDLR ndani ya jeshi lake (FARDC), jambo ambalo mataifa fulani ya nje yanalifumbia macho kwa maslahi yao.
Rais Kagame pia ameeleza kuwa kundi la FDLR limekuwa likijihusisha na uchimbaji wa madini kwa miaka mingi katika Mashariki mwa DRC, lakini halitajwi popote; badala yake lawama huelekezwa Rwanda. Amesema:
“Kwa nini wanachukuliwa kana kwamba hawana hatia katika matatizo haya, ilhali kila siku tunatoa ushahidi unaoonyesha uhusiano wa FDLR na machafuko haya? …
Ukweli ni kwamba baadhi ya wanachama wa FDLR wanajihusisha na uchimbaji wa madini Mashariki mwa Kongo. Wanayapeleka wapi madini hayo? Madini hayo hupitia Burundi na Uganda yanapelekwa Ulaya, lakini wao huishia kuilaumu Rwanda kwa kisingizio cha taarifa zinazotolewa kuhusu madini.”
Rais Paul Kagame, amesisitiza kuwa hakuna shaka kwamba kundi hilo lina idadi kubwa ya wapiganaji.
Ameonyesha pia kutoridhishwa na jinsi Burundi na Uganda zinavyoruhusiwa kutuma majeshi kupambana na makundi ya waasi ndani ya DRC, ilhali Rwanda huambiwa kimya kimya kwamba FDLR si tatizo.

Rais Paul Kagame akiwa kwenye kmkutano na waandishi wa habari
Rais Paul Kagame ametangaza kuwa mazungumzo yanayowahusisha wajumbe wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanayoendelea mjini Washington, Marekani, yanaendelea vizuri na yanaonyesha mwelekeo chanya wa kupatikana kwa amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu. Ameongeza
“Kuhusu uwezekano wa kukutana Washington, tukazungumza, tukakubaliana au hata tukatia saini baadhi ya makubaliano, hiyo ni hatua nzuri.
Ni hatua muhimu. Kwa miaka yote iliyopita, hakujawahi kutokea kitu kama hicho. Tulikuwa tunaona watu wakitembelea Rwanda na DRC, kisha wanakimbilia Umoja wa Mataifa, katika Baraza la Usalama, kutoa matamko na kupitisha maazimio.”

Waandishi wa habari wa Rwanda na Kimataifa kwenye mkutano
Mnamo tarehe 27 Juni 2025, Rwanda na DRC zilisaini makubaliano ya amani kwa usaidizi wa Marekani. Inatarajiwa kuwa makubaliano hayo yatafuatiwa na mengine kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika kuendeleza uchumi.
Marekani ilitamani kuona Rais Kagame na Rais Félix Tshisekedi wanakutana mwezi Oktoba mwaka 2025, lakini jambo hilo halikuwezekana.. Hata hivyo, inatarajiwa kuwa viongozi hao watakutana muda si mrefu.


Christopher Karenzi
