Rwanda ni mwenyeji wa mashindano ya kimataifa ya ndondi 2025.
Na Christopher Karenzi
Kwa mara ya kwanza kabisa, michuano ya nusu fainali za PFL (Africa Semifinals) zitafanyika jumamosi, tarehe 18 Otoba 2025 kwenye ukumbi wa BK Arena jijini Kigali, Rwanda.
Mpiganaji wa Rwanda, James Opio Bizimungu akiongea na vyombo vya habari jumatano tarehe 15 Octoba 2025 jijiji Kigali, amesema kuwa amejiandaa vizuri kuelekea pambano lake linalosubiriwa kwa hamu na wengi ambapo atachuana na mganda Isaac Omeda.
Akiongea na Brightafrica.rw Opio amesema kwamba amejipanga vizuri kuwakilisha vizuri Rwanda, amesema’’ Nimejitayarisha vizuri,yule ambaye tutapigana namfahamu na yeye pia najua amejiandaa lakini kutokana na matayarisho mazuri, pambano hili tutalishinda’’.Ameomba wanyarwanda waje kwa wingi kumshangilia ana imani watapandisha bendera ya Rwanda.

James Opio Bizimungu akiongea na vyombo vya habari
Kuhusu kiwango cha mchezo wa ndondi nchini Rwanda James Opio amesema kiwango kiko chini lakini kuna uwezekano wa kuinua huu mchezo, vijana wapo nimewaona tena wako tayari ‘’ Tuongeze nguvu vijana wapo wanaweza kucheza, nawaomba viongozi wa ngazi za michezo kama shirikisho la ndondi nchini Rwanda na washirika wao waweke bidii kuinua sekta ya mchezo huu naamini siku za usoni Rwanda tutafika mbali’’. Bizimungu amesema.
Professional FightersLeague (PFL) Africa Semifinals: Rwanda itajumuisha jumla ya mapambano 11, nane ni ya nusu fainali, mawili ya wachezaji mbadala, na moja kuonyesha uwezo (showcase fight).

Pambano kuu litawakutanisha bingwa kutoka Nigeria, mpiganaji mwenye mtindo wa kipekee katika uzito wa Featherweight Patrick Ocheme (7-1)dhidi ya mshambulizi hodari kutoka Burkina Faso Abdoul Razac Sankara (7-4), mwenye morali ya hali ya juu ambapo alishinda kwa “Knockout of the Night” huko Johannesburg, Afrika ya kusini.
Mbali na Uganda pamoja na Rwanda, mashindano haya yamewaleta pia wanandondi kutoka mataifa ya Cameroon, Zimbabwe, Nigeria, Guinea Konakry, Guinea Bissau, Ivory Coast, Senegal, Burkina Faso, Liberia, Algeria, Angola na Afrika ya Kusini.

Professional Fighters League (PFL) na Afro Nation, tamasha maarufu zaidi duniani la muziki wa Afrobeats, walitangaza ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu unaounganisha michezo ya ndondi mchanganyiko wa kiwango cha juu na jukwaa lenye ushawishi mkubwa wa kitamaduni barani Afrika.
Ushirikiano huu wa aina yake umetungwa ili kuonyesha nguvu, fahari na ubunifu wa vijana wa Kiafrika kupitia muunganiko wa michezo, muziki na mtindo wa maisha.
Ushirikiano huu ulianza kupitia shughuli kubwa za burudani zilizoongozwa na Afro Nation United katika matukio mawili ya kwanza ya PFL Africa jijini Cape Town tarehe 19 Julai na Johannesburg tarehe 9 Agosti na utahitimishwa na Fainali za PFL Africa mwezi Desemba mwaka huu.
Matukio haya yanajumuisha maonyesho ya moja kwa moja ya wasanii maarufu wa ndani na wa kimataifa, matukio ya kipekee kwa mashabiki, na sherehe za baada ya pambano ambazo hufikisha nguvu na ladha ya Afro Nation moja kwa moja kwenye ringi ya PFL.
