Mateka wa Israel wakabidhiwa Shirika la Red Cross

Share Now

Christopher Karenzi

Hamas imekabidhi mateka saba kwa Shirika la Msalaba Mwekundu Jumatatu, likiwa kundi la kwanza kuachiliwa chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas. Israel inapaswa kuwaachia mamia ya Wapalestin

Magari ya Shirika la Msalaba Mwekundu yakielekea mashariki mwa Gaza kutoka Khan Yunis, Oktoba 13, 2025, kabla ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel walioshikiliwa na Hamas tangu Oktoba 7, 2023.

Kulingana na DW, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) limesema Jumatatu kuwa limeanza “operesheni ya awamu nyingi” kusimamia mchakato wa kuwaachilia mateka waliokuwa wakishikiliwa na Hamas huko Gaza na wafungwa wa Kipalestina walioko mikononi mwa Israel.

Mabadilishano haya, yanayofanyika chini ya mpango wa kusitisha mapigano uliofadhiliwa na Marekani, yanaashiria hatua ya kwanza kubwa kuelekea kumaliza vita vya miaka miwili vilivyoiteketeza Gaza na kusababisha maafa makubwa pande zote mbili.

Mapema Jumatatu, Hamas ilitoa orodha ya mateka 20 walio hai watakaoachiliwa, pamoja na orodha ya zaidi ya wafungwa 1,900 wa Kipalestina wanaotarajiwa kuachiwa na Israel.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi (katikati) akikutana mjini Cairo na mjumbe wa Rais wa Marekani kwa masuala ya Mashariki ya Kati Steve Witkoff (wa tatu kushoto), mkwewe Jared Kushner (wa pili kushoto), na Balozi wa Marekani nchini Misri Herro Mustafa Garg. Misri itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa kujadili hatua zinazofuata za mpango wa amani wa Rais Trump.

Chini ya mpango wa Marekani, Gaza itasimamiwa na chombo cha kimataifa kitakachowezesha wataalamu wa Kipalestina kuendesha shughuli za kila siku, huku usalama ukisimamiwa na vikosi vya Kiarabu vitakavyopatiwa mafunzo na Misri na Jordan.

Hamas imesema haitasalimisha silaha, ikisisitiza kuwa utawala wa Gaza unapaswa kuamuliwa na Wapalestina wenyewe. Wakati huo, Israel imesisitiza kuwa amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila kuhakikisha Hamas inavunjwa kijeshi kabisa.

Makubaliano haya pia yameruhusu misaada mikubwa ya kibinadamu kuingia Gaza kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa. Umoja wa Mataifa umesema Israel imeidhinisha tani 190,000 za misaada kuingia, na malori 600 yanatarajiwa kuingia kila siku chini ya makubaliano mapya.

“Sehemu kubwa ya Gaza sasa ni jangwa,” amesema mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher, akibainisha kuwa mpango wa shirika hilo ni kurejesha huduma za msingi, kupeleka chakula, mafuta, na kuondoa vifusi ndani ya miezi miwili ijayo.

Jeshi la Israel limesema mateka hao wataanza kukabidhiwa kwa maafisa wa Msalaba Mwekundu kabla ya kupelekwa katika vituo vya kijeshi kwa uchunguzi wa afya na kuunganishwa na familia zao.

Magari ya Msalaba Mwekundu yalionekana yakisafiri kati ya Gaza na Israel, huku vyombo vya habari vya Israel vikiripoti moja kwa moja wakati familia zikiwa na hamu ya kusikia habari njema.

Mpango wa Marekani waweza kubadilisha uongozi wa Gaza

Rais wa Marekani Donald Trump aliwasili nchini Israel Jumatatu, ambako anatarajiwa kukutana na familia za mateka waliokuwa wakishikiliwa na kutoa hotuba katika bunge la Israel (Knesset) kabla ya kuelekea Misri kwa ajili ya mkutano wa amani wa kikanda.

Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi ataongoza mkutano huo kwa pamoja na Trump, akishirikiana na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas na viongozi wengine wa kimataifa.

Mazungumzo hayo yanakusudia kupanga mustakabali wa Gaza baada ya vita, ingawa bado kuna tofauti kubwa kuhusu nani ataongoza eneo hilo pindi jeshi la Israel litakapoondoka.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *