Naom Wafula aandika historia huku Nsanzuwera Akiendelea kutawala SportsBiz Africa Golf Championship
Na Christopher Karenzi
Mashindano ya SportsBiz Africa Golf Championship yameandelea alhamisi tarehe 4/9/2025 katika viwanja vya jiji la Kigali Golf Resort & Villas ambapo yameshuhudia matukio ya kipekee.
Wafula Aangaza kwa Shimo la Ajabu
Mkenya Naom Wafula ameandika historia baada ya kufunga shimo kwa risasi moja(hole-in-one) kwenye shimo la pili la par-3. Tukio hilo limemtia nguvu na kumsaidia kurekodi alama ya 4 chini ya par 68, na kufikisha jumla ya 1 juu ya par145 baada ya raundi mbili. Wafula sasa yupo miongoni mwa wachezaji 30 bora waliopenya hatua ya mwisho. “Nilipoona mpira wangu umeingia moja kwa moja nilifurahi sana, lakini caddie wangu akanikumbusha bado nina mashimo mengi ya kucheza. Ujasiri huo ndiyo ulinisaidia kumaliza vizuri,” alisema Wafula baada ya raundi hiyo.
Nsanzuwera Afurahisha Mashabiki wa Nyumbani

Nyota wa Rwanda Celestin Nsanzuwera alidhihirisha ubora wake kwa kupiga birdie tisa na eagle moja, akimaliza na alama bora ya 9 chini ya par 63. Baada ya raundi mbili, Nsanzuwera anaongoza mashindano kwa jumla ya 13 chini ya par131, akiwacha washindani wake kwa pengo la alama saba.
“Siku ya leo nilibaki mtulivu, nikaanza na birdie mbili kisha eagle, na hapo nikajua nina nafasi kubwa. Kwa kuwa huu ni uwanja wangu wa nyumbani, nimeutumia ipasavyo. Ijumaa hii mpango ni ule ule, kubaki makini na kuamini putts zangu,” alisema Nsanzuwera.

Celestin Nsanzuwera akichapa kazi
Aidha kwa wachezaji wengine katika nafasi ya pili kwa pamoja wakiwa na 6 chini ya par 138 ni Travis Procter (Afrika Kusini) na bingwa wa DP World Tour mara mbili Haydn Porteous. Procter na Porteous wote walimaliza leo na alama ya 3 chini ya par 69.
Miongoni mwa Wakenya, Eric Ooko aling’ara zaidi kwa raundi ya 2 chini ya par 70, akimfikisha jumla ya 5 chini ya par 139, hatua moja tu nje ya tatu bora. Wakenya wengine waliopenya ni pamoja na John Wangai, Jastas Madoya, Dismas Indiza, Mutahi Kibugu, Samuel Njoroge, Michael Karanga, John Lejirma, David Wakhu, Ken Abuto, Greg Snow, Daniel Nduva, Mohit Mediratta, Jacob Okello, na Njoroge Kibugu.
Mchujo uliwekwa kwenye alama ya 3 juu ya par 147, na wachezaji 30 pekee sasa wamesalia kupigania dola za Marekani 25,000, pamoja na pointi muhimu za Sunshine Development Tour, OWGR, na WAGR.
Ni mashindano ya kimataifa yaliyoanza Jumatano tarehe 3 Septemba kwenye Kigali Golf Resort & Villas, kupitia Sunshine Development Tour, mashindano ambayo kawaida huwakutanisha wachezaji wa gofu kutoka Afrika Kusini na Afrika Mashariki, yakiwa ni mara yake ya tano. Mashindano haya yamewaleta kwa pamoja wachezaji 120 wa gofu waliobobea, kutoka nchi 16 tofauti, na yatasaidia pia kuongeza alama kwenye viwango vya kimataifa.
Mashindano haya yameandaliwa na pia kuunganishwa na mkutano wa biashara na michezo uitwao SportsBiz Africa Forum, utakaofanyika nchini Rwanda, Kigali kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 10 Septemba 2025 katika Kigali Convention Centre.
