Rais Kagame azungumza na Touadéra kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Rwanda na Afrika ya Kati
Na Christopher Karenzi
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Touadéra, ambaye amefanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Rwanda iliyoanza Jumapili, tarehe 23 Novemba 2025.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika jioni ya Jumapili, viongozi hao wawili walijadili hatua za kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya mataifa yao, hususan katika sekta ya usalama. Rwanda imeendelea kutoa mchango mkubwa nchini Afrika ya Kati kupitia wanajeshi wake wanaoshiriki katika operesheni za kurejesha na kudumisha amani, kwa mujibu wa makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama pamoja na majukumu ya MINUSCA chini ya Umoja wa Mataifa.

Rais Touadéra alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali na Waziri wa Usalama, Dkt. Vincent Biruta, ikiwa ni ishara ya kuendelezwa kwa uhusiano mzuri uliopo kati ya mataifa haya mawili.
Kwa miaka kadhaa sasa, Rwanda imekuwa mshirika muhimu wa Afrika ya Kati katika juhudi za kuimarisha utulivu, kulinda viongozi wakuu wa nchi hiyo, na kutoa ulinzi katika maeneo muhimu ya taifa. Jeshi na Polisi ya Rwanda pia hutajwa kwa uhusiano mzuri inaoujenga na wananchi wa Afrika ya Kati kupitia majukumu yao ya kila siku.
Mbali na usalama, viongozi hao walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika maeneo mengine yakiwemo biashara na uwekezaji, sekta ya fedha, utamaduni, na kubadilishana ujuzi.

Rais wa Afrika ya Kati Faustin-Archange Touadéra, akipokewa kwenye Ikulu ya Rais na mwenyeji wake Rais Paul Kagame
Aidha, jumuiya ya Warwanda wanaoishi na kufanya kazi nchini Afrika ya Kati, wakiwamo wale wanaohudumu katika operesheni za kulinda amani, imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kuadhimisha sikukuu mbalimbali kwa ushirikiano na Ubalozi wa Rwanda mjini Bangui.
Uhusiano kati ya Rwanda na Afrika ya Kati unaendelea kuchukuliwa kuwa mfano wa ushirikiano wa Afrika unaolenga kutatua changamoto za bara hili katika nyanja za amani, usalama na maendeleo endelevu.
