Betty Kibaara: Wanafunzi milioni 65 barani Afrika hupewa chakula mashuleni
Rwanda imekuwa mwenyeji wa Kongamano la Mfumo wa Chakula Barani Afrika 2024. Zaidi ya wadau 4,500 kutoka mataifa mbali mbali barani Afrika wameshiriki Kongamano hilo kuanzia tarehe 2-6 Septemba 2024 jijini Kigali, Rwanda.
Betty Kibaara ni Mkurugenzi wa Mpango wa Chakula katika Shirika la The Rockefeller Foundation, Ofisi ya Kanda ya Afrika, alikuwa mongoni mwa walioshiriki kongamano hili.
Betty Kibaara ni mkenya anayeongoza uwekezaji wa Shirika hilo katika kubadilisha mifumo ya chakula pamoja na kuongeza upatikanaji wa vyakula vya lishe kupitia programu za chakula shuleni.
Nimeanza kumuuliza umuhimu wa kuwekeza mashuleni barani Afrika, kwa kuzingatia faida za lishe, elimu na kiuchumi?
Amesema kwamba chakula kwa watoto ni muhimu sana akieleza takwimu zilivo mashuleni “Wanafunzi milioni 65 barani Afrika hupewa chakula mashuleni. Tunapozungumza hiyo idadi barani Afrika kwa wanafunzi wanaopata mlo shuleni bado hawatoshi. Amesema Mkurugenzi Betty Kibaara.

Mkurugenzi wa Shirika la The Rockefeller Foundation Betty Kibaara
Mkurugenzi Kibaara ametoa mfano jinsi alivofaidika enzi za aliyekuwa Rais wa zamani wa Kenya Hayati Daniel Toroitich Arap Moi. Wanafuzi walikuwa wakipata maziwa maarufu “ Maziwa ya Nyayo’’. Amebaini kuwa watoto wapatao milioni 4 walipata maziwa kutokana na mpango wa Nyayo wakati huo nchini humo.
Uwekezaji huu ulichochea sekta ya maziwa na kuchangia ukuaji mkubwa na kuifanya Kenya kuwa inaongoza katika sekta ya maziwa. Hebu fikiria kama tungeweza kufanya vivyo hivyo kwa minyororo mingine ya thamani kama vile mtama.
Bi Kibaara amesema miaka miwili iyopita baadhi ya serikali zinasaidia watoto kuhakikisha wanapata chakula kupitia Muungano wa Elimu Ulimwenguni ” Global School Meals coalition”. “Nchi 100 zimesaini mkataba wa kuunga mkono pendekezo hilo ambapo nchi 40 barani Afrika zimethibitisha kwamba zitaweka mikakati kuhakikisha kwamba watoto wanapewa vyakula shuleni. Nchi hizo ni kama Rwanda, Kenya , Uganda na Tanzania ’’.
Mkurugenzi Kibaara hata hivo ana hofu kwamba baadhi ya mataifa yanahitaji kutimiza ahadi lakini kupata fedha ya kutosha kwa kila mtoto kupata chakula si rahisi.

Watu mbali mbali wakitemblea Banda la bidhaa za Shirika la Rockefeller Kigali. Bidhaa hizo ni kama unga wa posho ambao umesagwa bila kutoa pumba na vijidudu na nafaka nzima.
Kiongozi wa Shirika la The Rockefeller ameongeza kwamba lengo hasa la Shirika hilo ni kuhakikisha kwamba wanaongea na viongozi wa serikali mbali mbali na kujadiliana ni wapi pesa zinaweza kupatikana kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
Kongamano hili kubwa hufanyika kila mwaka mwezi Septemba, linajikita hasa kuhusiana na sekta ya kilimo ambapo linawaleta kwa pamoja watu tofauti taofauti, wajumbe kutoka serikalini, mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s na watu binafsi ili kujadiliana juu ya changamoto wanazopitia barani Afrika.




Christopher Karenzi
