Simba Queens yapangwa na Kenya Police Bullets katika mechi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake

Share Now

Na Karenzi Christopher

Timu ya Tanzania ya Simba Queens FC imepangwa kukutana na Kenya Police Bullets FC katika michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake ya ukanda wa CECAFA mwaka 2026.

Droo rasmi ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda.  Droo hiyo iliendeshwa na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya  CECAFA, Andrew Jackson Oryada, akisaidiwa na aliyekuwa mchezaji wa kimataifa wa Rwanda, Gloria Sofia Nibagwire.

Michuano hiyo ya kufuzu, ambayo itashirikisha timu 10, itafanyika Kigali kuanzia Agosti 21 hadi 31, 2026. Mechi zitachezwa katika Kigali Pele Stadium na uwanja wa FERWAFA Technical Centre.

Simba Queens, ambao walikuwa mabingwa wa ukanda wa CECAFA mwaka 2022, wamewekwa Kundi C, pamoja na mabingwa wa Kenya, Kenya Police Bullets, na Top Girls Academy kutoka Burundi.

Wenyeji Rayon Sport WFC wamewekwa Kundi A pamoja na Yei Joint Star FC ya Sudan Kusini, Mafunzo SC ya Zanzibar na Denden FC ya Eritrea.

Commercial Bank of Ethiopia (CBE), ambao wamefika fainali mara mbili na kutwaa ubingwa mwaka 2024, wamewekwa Kundi B pamoja na Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FC Ujeco ya Djibouti.

Timu mbili bora kutoka Kundi A, pamoja na vinara wa Kundi B na Kundi C, zitafuzu hatua ya nusu fainali.

Katika hatua ya nusu fainali: Mshindi wa Kundi B atacheza dhidi ya mshindi wa pili wa Kundi A. Mshindi wa Kundi A atakutana na mshindi wa Kundi C.

Bingwa wa michuano hiyo ya CECAFA ataiwakilisha kanda ya CECAFA katika Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake 2026.

Kundi A  kuna Rayon Sport WFC , Yei Joint Star FC , Mafunzo SC na Denden FC

Kundi B: CBE FC , Kawempe,  Muslim Ladies na FC Ujeco

Kundi C: Simba Queens , Kenya Police Bullets FC na Top Girls Academy FC

Kwa sasa, CAF bado haijatangaza rasmi uwanja na tarehe za kuanza kwa Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake 2026.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *