Rais Kagame: Ushirikiano kati ya Jeshi la Rwanda na wananchi uliwezesha kuwashinda waasi (abacengezi)

Share Now

Christopher Karenzi

Rais wa Jamhuri, Paul Kagame, amesema kuwa utamaduni na mwenendo unaoonekana katika Jeshi la Rwanda la sasa umetokana na nyakati hizo ngumu, na kwamba ni miongoni mwa majeshi bora duniani kwa weledi na kujitolea kwa hali ya juu.

Alipokuwa akihutubia washiriki wa hafla ya kuanza Wiki ya Maombolezo na siku 100 za kumbukumbu ya mara ya 32 ya Jenoside yakorewe Abatutsi mu 1994, Rais Kagame alisema hakuna adhabu wala matusi yanayoweza kupunguza hadhi ya Jeshi la Rwanda. Alieleza kuwa Wanyarwanda walijifunza somo zito, lenye maumivu na lisilosahaulika, kutokana na ukweli kwamba walitelekezwa na mataifa ya nje kwa sababu maisha yao hayakuwa na maslahi kwa wengine.

 “Ndiyo maana ilikuwa lazima Jeshi la RPA liongoze mapambano ya kusitisha mauaji ya kimbari, na kweli likayasitisha. Kinachotuhuzunisha zaidi ni kwamba hatukuweza kufika kila mahali palipokuwa panatekelezwa mauaji hayo kwa wakati.” Amesema.

Aliendelea kukosoa baadhi ya watu ambao bado hawana utayari wa kukubali na kusema ukweli ulivyo, kwa sababu ambazo hata sisi hatuzielewi. Aliongeza kuwa hadi leo, mafunzo yaliyotokana na historia ya mauaji ya kimbari yanaongoza mwenendo wa Jeshi la Rwanda, iwe ndani ya nchi au katika misheni za kulinda amani nje ya nchi, na limeendelea kuheshimiwa kwa namna linavyotekeleza majukumu yake.

Alisema: “Kwa kweli, hakuna adhabu wala matusi kutoka popote pale yanayoweza kupunguza heshima na uadilifu wa Jeshi na vyombo vya usalama vya Rwanda; ni miongoni mwa vilivyo bora zaidi duniani. Natarajia kuuliza viongozi wengine wa juu duniani ili kuelewa msingi wa dhuluma kama hii.”

Rais Kagame alisema Wanyarwanda wanaelewa vizuri gharama ya kuvumilia itikadi kali, ndiyo maana msingi wa sera ya usalama ni kulinda maisha ya raia walio hatarini. Alieleza kuwa baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Wanyarwanda waliamua kujenga nchi yao bila ubaguzi, na wakaazimia kutoruhusu tena siasa za mauaji ya kimbari kupata nafasi nchini Rwanda.

Aliendelea kusema: “Katika safari hii, Wanyarwanda tumekutana na wakosoaji wa juhudi zetu na wanaopotosha historia yetu mara nyingi. Lakini nguvu yetu ya kudumu ni kutumia akili zetu kutafuta ukweli na kutumia sauti zetu kusema tunapoona mambo hayaendi sawa. Tunapaswa kueleza wazi hatari tunazoziona bado zipo.”

Alifafanua pia kuwa majeshi ya serikali iliyopanga na kutekeleza mauaji ya kimbari yalitorokea Zaire, ambayo sasa ni Repubulika Iharanira Demokarasi ya Congo, pamoja na raia wengi, ambapo walijipanga upya na kuunda kundi la kigaidi la FDLR ambalo hadi leo linaendelea kuhatarisha usalama wa eneo hilo na kusambaza itikadi ya mauaji ya kimbari.

Rais Kagame alisema ushirikiano kati ya Jeshi la Rwanda na wananchi uliwezesha kuwashinda waasi (abacengezi) kati ya mwaka 1996 hadi 1999, lakini changamoto za usalama ziliendelea kuwepo, hivyo hatua za ulinzi zikaimarishwa ili kuzuia hatari kutoka kwa FDLR.  “Tangu wakati huo, mikakati yetu ya ulinzi inatuwezesha kujilinda na kulinda nchi yetu, tukihakikisha kuwa mashambulizi kama hayo hayatatokea tena kutoka nje ya mipaka yetu. Hili si tatizo ambalo Rwanda inapaswa kushughulikia peke yake. Kufanya hivyo ni kuwapa nafasi wale wanaochochea matatizo, wakati Rwanda inaadhibiwa kwa kujilinda.” Rais Kagame aliongeza kuwa kulinda uhuru wa Afrika kunapaswa kwenda sambamba na taasisi za Afrika kuchukua maamuzi sahihi na ya haraka pale Waafrika wanapokuwa hatarini. Pia alisisitiza kuwa wahalifu hawapaswi kujificha nyuma ya dhana ya uhuru wa nchi ili kukwepa kuwajibika kwa uhalifu wao au kunyima wananchi haki zao.

Alionya kuwa iwapo itikadi ya mauaji ya kimbari inayoendelea kusambaa katika ukanda ikiwa haitadhibitiwa, inaweza kulirudisha nyuma tena eneo hilo.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *