”Usafi uwe utamaduni” Nkundwanabake, Kiongozi wa Eco-stewardship Generation (ESGEN)
Na Christopher Karenzi
Nkundwanabake Cedrick, ni kiongozi wa Eco-stewardship Generation (ESGEN) nchini Rwanda, akishirikiana na vijana wa Tarafa ya Kanyinya, Wilaya ya Nyarugenge jijini Kigali, ameanzisha mradi unaolenga kudhibiti usafi wa mito.

Nkundwanabake Cedrick, kiongozi wa Eco-stewardship Generation (ESGEN)
Akizungumza na Brightafrica.rw, ameeleza kuwa sehemu nyingi za mito zimeathirika kutokana na mmomonyoko wa udongo kutoka milimani, miti inayoanguka, na mawe makubwa kuingia kwenye mito. Moja ya shughuli kuu wanazofanya hasa ni kuondoa taka za plastiki kwenye Mto Nyabarongo na kufanya usafi wa mazingira ya maji.
Amesema: “Mbali na shughuli hizo, tunapanga programu kwenye shule kwa ajili ya kusimamia taka na kuhakikisha hazisambazwi hovyo shuleni. Pia tunafundisha wanafunzi kutenganisha taka zinazooza na zisizooza, ili wajifunze jukumu la kuzidhibiti.”
Kuhusu ushirikiano na Taasisi ya Mazingira nchini Rwanda (REMA), Nkundwanabake amesema kuwa bado hawajaanza kushirikiana kikamilifu, ingawa waliwahi kutembelewa na viongozi wa taasisi hiyo. “Mbali na uongozi unaofatilia tunayofanya, mara nyingine tunategemea vifaa vya msaada vinavyopatikana kupitia mipango ya serikali,” ameeleza.
Ameongeza kuwa mwaka 2021 ndipo walianza rasmi shughuli za kusafisha mito na mabwawa, wakianzia maeneo yanayozunguka sehemu zao za kazi. Lengo lao kuu ni kuhakikisha kuwa usafi unazingatiwa si tu majini, bali pia mashuleni na sehemu nyingine, ambapo wanafunzi na jamii wanajifunza namna ya kushughulikia taka kwa njia sahihi.

Mwaka huo huo wa 2021, walishirikiana na vijana wa Wilaya ya Rulindo kufanya usafi kwenye mito, wakiondoa plastiki na kuzitupa kwenye masoko yaliyoko maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Walianzia katika Murenge wa Ngoma, karibu na Shyorongi, na baadaye wakaendelea hadi Kijabagwe, pia ndani ya Rulindo.
Nkundwanabake amebaini kuwa wana ushirikiano wa kimataifa na Taasisi ya River Cleanup kutoka Ubelgiji, na yeye ndiye mwakilishi wa mpango wa “Let’s Do It Rwanda” (kwa Kiswahili: “Tufanye”).
Bwana Cedrick Nkundwanabake ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za kitaifa na Kimaataifa zinazohusika na mazingira kutoa ushirikiano na msaada wa hali na mali hususan kupewa vifaa ambavyo bado hawana, ili kuimarisha juhudi za kulinda mito na mazingira kwa ujumla.

Nkundwanabake Cedrick aliyevaa T-shirt nyeupe (katikati) akiwa pamoja na vijana

Vijana wakiondoa takataka kwenye mto
