Kenya yatoa hati ya kukamatwa kwa mwingereza anayetuhumiwa katika mauaji ya Agnes wanjiru

Share Now

Mwandishi wa Brightafrica

Nairobi, Kenya – Mahakama Kuu nchini Kenya imetoa hati ya kimahakama ya kumkamata raia wa Uingereza anayetuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Agnes Wanjiru, mwanamke mwenye umri wa miaka 21 aliyeuawa mwaka 2012 katika mji wa Nanyuki.

Mwili wa marehemu Wanjiru uligunduliwa baada ya miezi mitatu, ukiwa umewekwa ndani ya tanki la majitaka katika eneo la hoteli moja karibu na kambi ya kijeshi ya Uingereza iliyo katika mji huo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Wanjiru alionekana mara ya mwisho akiwa katika tafrija pamoja na wanajeshi wa Uingereza kabla ya kifo chake.

Jaji Alexander Muteti wa Mahakama Kuu alisema kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha unaoonyesha msingi wa kisheria wa kumfikisha mshukiwa mbele ya mahakama za Kenya ili ajibu mashtaka dhidi yake.

Kwa mujibu wa BBC, hatua hii imeelezwa kuwa ya kihistoria na muhimu na wakili wa familia ya marehemu, Bw. Kamau Mbiu, ambaye amesema kuwa sasa njia imefunguliwa rasmi kwa mchakato wa kisheria wa kumrejesha mshukiwa kutoka Uingereza. “Tumefurahishwa na uamuzi huu wa mahakama, lakini tunasisitiza kuwa mchakato mzima ufanyike kwa uwazi na kwa manufaa ya wananchi wote,” alisema Bw. Mbiu

Mchakato wa uhamishaji wa mshukiwa kutoka Uingereza sasa unatarajiwa kuanza rasmi, huku familia ya Wanjiru pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu wakiendelea kushinikiza haki kutendeka katika kesi hii iliyodumu kwa zaidi ya muongo mmoja bila hatua madhubuti.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *