Rais Kagame akiwa Dakar kwa ajili ya mkutano wa chakula barani afrika
Na Karenzi Christopher
DAKAR – Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, aliwasili jijini Dakar, Senegal, siku ya Jumapili, kwa ajili ya kushiriki kwenye mkutano mkubwa wa mwaka unaojadili masuala ya mnyororo wa thamani wa chakula barani Afrika. Mkutano huo umeanza rasmi tarehe 31 Agosti na unatarajiwa kufungwa tarehe 5 Septemba 2025.
Rais Kagame alipokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ambaye ni mmoja wa waandaaji wakuu wa mkutano huo. Tukio hili linatajwa kuwa la kihistoria kwani ni mara ya kwanza mkutano huu mkubwa kuandaliwa barani Afrika kwa kiwango hiki cha ushirikiano.
Mkutano huu unaleta pamoja viongozi wa serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, wanasiasa, watafiti, washirika wa maendeleo, pamoja na vijana wabunifu waliopo mstari wa mbele katika kuendeleza mnyororo wa chakula na kilimo barani Afrika.
Leo, Jumatatu, Septemba 1, Rais Kagame ameshiriki mkutano maalum unaowaleta pamoja viongozi vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaojihusisha na sekta ya kilimo na chakula. Mkutano huo unalenga kukuza uongozi wa vijana katika kuleta mageuzi ya kilimo chenye tija na endelevu.
Kwa mujibu wa waratibu, mkutano wa mwaka huu unashughulikia kwa kina kaulimbiu isemayo: “Vijana wa Afrika wanaongoza Ushirikiano, Ubunifu na Utekelezaji wa Maendeleo ya Mnyororo wa Kilimo na Chakula.”

Wachambuzi wa masuala ya kilimo wanasema kuwa mkutano huu ni fursa muhimu ya kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha bara la Afrika linajitegemea kwa chakula na pia linakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje.
Mkutano huu ulikuwa ukifahamika kama AGRF (African Green Revolution Forum) na ulianzishwa kwa mara ya kwanza nchini Rwanda. Uliibuliwa kwa nia ya kuongeza msukumo wa kisiasa, kuharakisha utekelezaji wa sera na kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo, ili kufanikisha mnyororo wa chakula wenye tija na usio wa kibaguzi.
Matarajio ni kwamba majadiliano ya mwaka huu yataibua maazimio makubwa yatakayosaidia kubadilisha sura ya kilimo barani Afrika, hasa kwa kuimarisha nafasi ya vijana katika sekta hii muhimu.

