Wachezaji 60 Kutoka Nchi 21 Barani Afrika wakutana Kambini jijini Kigali
Na Christopher Karenzi
Toleo la 21 la Basketball Without Borders (BWB) Afrika limeanza rasmi jijini Kigali, Rwanda, likiwa na msisitizo mkubwa wa kuhimiza ushiriki wa wasichana katika mchezo wa mpira wa kikapu barani Afrika.
Kwa mara ya kwanza, katika Afrika ya Mashariki na Kati, Rwanda ni mwenyeji wa kambi ya mchezo wa mpira wa kikapu maarufu Basketball Without Borders (BWB) inayokutanisha vijana 60 wenye umri wa miaka 18 na chini kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika.
Kambi hii, ambayo ni ya 21 tangu kuanzishwa kwake na hufanyika katika sehemu tofauti duniani, imeanza leo Jumamosi tarehe 23 Agosti itatamatika hadi Jumanne tarehe 26 Agosti 2025 kwenye viwanja vya ndani vya Petit Stade na BK Arena, jijini Kigali, Rwanda.
Basketball Without Borders ni mpango ulioanzishwa kwa ushirikiano kati ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Kikapu (FIBA), ukiwaleta pamoja vijana wenye vipaji vinavyoahidi, kuwapatia mafunzo kutoka kwa makocha, wachezaji mashuhuri na nyota wa NBA pamoja na WNBA.

Washiriki hao wanajifunza mbinu na uzoefu kutoka kwa wachezaji wa sasa na wa zamani wa NBA na WNBA, pamoja na makocha mashuhuri.
Miongoni mwa viongozi na wakufunzi waliopo ni pamoja na Clare Akamanzi, Mkurugenzi Mtendaji wa NBA Africa,Michael Finley, Mkuu wa NBA nchini Kenya Troy Justice, Mkuu wa Operesheni za Mpira wa Kikapu Kimataifa na Kita Matungulu, Mkurugenzi wa Operesheni za NBA Africa.
Kambi hii ya Basketball Without Borders inatarajiwa kutoa nafasi kwa vijana wa Kiafrika kukuza vipaji vyao na pia kujifunza nidhamu, uongozi na mshikamano kupitia mpira wa kikapu.
Akizungumza katika mahojiano wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBA Afrika, Clare Akamanzi, alisema kuwa kambi ya BWB Afrika ni fursa ya kuwaonyesha wasichana vijana kuwa kuna nafasi kwao katika mchezo wa mpira wa kikapu.
“Kwa sababu, ingawa michezo kwa ujumla imejaa wanaume, wasichana wengi zaidi sasa wanapata taaluma nzuri kupitia mpira wa kikapu na michezo kwa ujumla. Na programu kama BWB ni njia ya kuwaonyesha wasichana kwamba nao wanaweza kucheza mpira wa kikapu. Na wanaweza kucheza kwa mtindo wao wenyewe,” alisema.
Fursa ya Uongozi na Maendeleo ya Kibinafsi

Mbali na mafunzo ya mchezo, washiriki watapata nafasi ya kushiriki warsha za uongozi, mafunzo ya maisha, na shughuli za kijamii kama: Kliniki ya mpira wa kikapu kwa walemavu kwa kushirikiana na FERWABA, Programu ya Shooting Touch kwa wanawake wazee
Kambi hiyo ya siku kadhaa imekusanya wachezaji 60 wa kiume na wa kike wa umri wa shule ya sekondari kutoka nchi 21 mbalimbali barani Afrika. Washiriki hao wanapata mafunzo kutoka kwa wachezaji na makocha maarufu wa NBA na WNBA.
Rwanda, mwenyeji wa tukio hilo, inawakilishwa na wachezaji wanne:Liliane Ingabire, Plamedie Bizimana Kayira, Sean Mwesigwa na Gabriel Ndoba.
Ni mara ya kwanza kambi hii kufanyika Afrika Mashariki, kwani hapo awali iliandaliwa katika nchi za Angola, Misri, Senegal na Afrika Kusini.
