Kuipenda nchi ndiyo nguzo ya kwanza ya RDF: Brigedia Jenerali Rwivanga
Na Christopher Karenzi
chriskarenzi@gmail.com
Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga, msemaji wa Jeshi la ulinzi la Rwanda (RDF) alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu Maadhimisho ya siku ya uzalendo yanayofanyika kila mwaka Oktoba Mosi, amesema kuwa Tarehe 1 Oktoba 1990 ni siku iliyozindua harakati za ukombozi wa taifa ambalo lilikuwa likiongozwa vibaya kwa miongo mitatu.
Kwa mujibu wa Brig. Gen. Rwivanga, maana ya uzalendo kwa mtazamo wa RDF inajengwa juu ya misingi ya maadili yake, historia ya kujitolea kwake, na wajibu wa kutekeleza ndani na nje ya Rwanda, ikiwemo operesheni katika nchi ya Msumbiji na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Amesema: “Jeshi la Rwanda lina mshikamano na ujasiri wa kweli wa kulinda taifa na kulitolea mhanga. Ni kujitolea kulinda maslahi ya taifa letu, ardhi yake, na kuendeleza malengo ya mshikamano na maendeleo.”
Maadili ya msingi ya uzalendo

Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga, msemaji wa Jeshi la ulinzi la Rwanda (RDF
Brig. Gen. Rwivanga amebainisha kuwa uzalendo hauhusiani tu na vita, bali pia maadili kama kujitolea katika kazi, kuheshimu wengine, kuwa jasiri nyakati ngumu, tabia njema na mshikikano wa kijamii.“Kwa kifupi, kulipenda taifa ndilo nguzo ya kwanza ya RDF, lakini pia tunaweka mbele maadili mengine kama uaminifu, kujitolea kwa wengine bila kutafuta maslahi, uwazi, na kuwa tayari kujitoa mhanga. Maadili haya yote yameunganishwa na dhana ya kulipenda taifa.”Amesema Brig.Gen. Rwivanga
“Lengo letu si kufa”
Alipoulizwa namna ambavyo uzalendo hupimwa katika RDF, Brig. Gen. Rwivanga ameeleza kuwa unadhihirishwa kwa matendo ya askari au hata raia wa kawaida.
Amefafanua kuwa: “Ni kulitumikia taifa lako kwa njia mbalimbali. Si lazima uwe jeshini. Pia ni kulinda taifa lako na wakati mwingine kuwa tayari kutoa jasho, muda, mali, au hata damu yako kwa ajili yake.”
Akinukuu maneno ya Jenerali George S. Patton Jr. wa Marekani katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, amesema: “Lengo letu si kufa. Wajibu wa mwanajeshi si kufa kwa ajili ya taifa lake, bali kulinda taifa na wananchi wake.”
Aidha ameongeza kuwa askari hulazimika kulipa gharama ya mwisho kwa ujasiri: “Wakati mwingine kiongozi anaweza kuamua kuweka maisha yake hatarini ili kulinda wenzake. Mfano, kukumbatia bomu la mkono (grenade) ili kuokoa wenzako wengi wasiangamie. Huo ndio mhanga wa juu kabisa wa uzalendo.”Amenena Brig.Gen. Rwivanga
