APR FC yashindwa kutamba nyumbani mbele ya mafarao wa Pyramids
Na Christopher Karenzi
APR FC yafungwa na Pyramids FC 2-0 katika mchuano wa kwanza wa mtoano wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2025
Mchezo huu umefanyika Jumatano, tarehe 1 Oktoba 2025 saa nane mchana kwenye Uwanja wa Kigali Pele Stadium.
Mashabiki wa APR FC walianza kwa hamasa kubwa, huku timu ya Majeshi ikishambulia mara kwa mara kupitia upande wa kushoto palipokuwa na Mugisha Gilbert, na kusababisha wachezaji wa Pyramids FC kufanya makosa yaliyowapa kadi za njano.
Kadri dakika zilivyozidi kusonga, Pyramids FC walizidi kuingia kwenye mchezo, ambapo Abdelrahman Mohamed alitoa shuti kali lililopaa nje ya mlindamlango AHMED NASER MAHMOUD MOAWAD ELSHENAWI.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare tasa ya 0-0. Kipindi cha pili, APR FC walipoteza nafasi ya wazi baada ya krosi ya Ruboneka Jean Bosco kupokelewa na William Togui kwa kichwa, lakini kipa wa Pyramids FC akaokoa. Dakika ya 39, William Togui alimpa pasi nzuri Mugisha Gilbert ambaye alipiga shuti kali lililopishana kidogo na goli.

Fiston Kalala Mayele akiwa pamoja na wenzake
Baada ya dakika mbili tu, mshambuliaji hatari wa Pyramids FC, Fiston Kalala Mayele, alifungua ukurasa wa mabao baada ya Niyomugabo Claude kupoteza mpira, ameachia mkwaju, kipa Ishimwe Pierre akashindwa kuuzuia litatinga bao la kwanza.
APR FC waliendelea kutafuta bao la kusawazisha lakini kipa wa Pyramids FC Elshenawi aliendelea kuwa mwiba.
Kiungo mshambuliaji wa APR FC Memel Dao wa alipiga shuti kali lakini kipa akaokoa hatari. Dakika ya 70, kocha wa Pyramids FC, Krunoslav Jurcic, alionyeshwa kadi nyekundu kwa kuonyesha kutoridhishwa na maamuzi ya waamuzi.

Mayele akikabiliana vikali na beki wa APR Clement
Kocha wa APR FC alifanya mabadiliko kwa kuwatoa William Togui na Mugisha Gilbert na kuwaleta Mamadou Sy na Denis Omedi. Mabadiliko haya yalileta uhai kwenye mashambulizi, na hata Mamadou Sy alifunga bao lililokataliwa kwa kuwa alikuwa ameotea.
Dakika ya 85, Fiston Kalala Mayele tena akafunga bao la pili la Pyramids FC baada ya wachezaji wa APR FC kupoteza mpira, na shuti lake likatikisa nyavu,
Mchezo ukamalizika kwa APR FC kupoteza 2-0, matokeo ambayo yanaifanya kuwa na mtihani mgumu kwani ili kusonga mbele itahitajika kushinda kwa mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano. Mchuano wa marudiano umepangwa kuchezwa Jumapili, tarehe 5 Oktoba 2025 saa moja jioni kwenye Uwanja wa 30 June Stadium huko Misri.

