Siku ambayo Habyarimana aliipokea Rayon Sports na kutoa ishara za mpango wa mauaji ya kimbari
Waziri wa Umoja wa Wanyarwanda na Uraia, Bizimana Jean Damascène, amesema kuwa mwezi Machi 1994, aliyekuwa Rais wa Rwanda wakati huo, Juvenal Habyarimana, alipokuwa akiipokea timu ya Rayon Sports, alionyesha dalili za mpango wa mauaji ya kimbari ambao serikali yake ilikuwa inapanga dhidi ya Watutsi.
Wakati huo, Habyarimana aliwapokea wachezaji na makocha wa Rayon Sports katika hoteli ya Horizon iliyoko mlimani Rebero, jijini Kigali baada ya timu hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika na kuiondoa Al-Hilal ya Sudan.
Waziri Bizimana alisema kuwa katika hafla hiyo, Habyarimana alizungumza maneno yaliyokuwa na ishara za mauaji ya kimbari.
Aliandika kwenye ukurasa wake wa X akisema:
“Tarehe 20 Machi 1994, Rais Habyarimana aliipokea Rayon Sports mjini Kigali kwenye uwanja wa ndege wa Kanombe, kisha wakaenda katika hoteli yake ya Rebero L’Horizon. Huko alitoa hotuba na kuonyesha dalili za mauaji ya kimbari.
Aliwaambia kuwa hajawahi kushindwa maishani, na alipokuwa akicheza mpira alikuwa beki, na hakuna mchezaji aliyewahi kumpita kwa sababu hakuwa anaogopa kumvunja mguu.”
Aliendelea kusema:
“Maneno haya aliyasema wakati tayari alikuwa amekataa kuunda serikali ya mpito kama ilivyokubaliwa katika Makubaliano ya Amani ya Arusha.
Pia, tarehe 18 na 19 Machi 1994, Waziri Mkuu aliyeteuliwa, Faustin Twagiramungu, pamoja na Waziri Mkuu wa wakati huo, Agathe Uwilingiyimana, walikuwa tayari wamempa Rais Habyarimana orodha ya mawaziri na wabunge waliopaswa kuingia katika serikali hiyo ya mpito.”
Bottom of Form
Bizimana alisema kuwa maneno ambayo Rais Juvenal Habyarimana aliyasema tarehe 20 Machi 1994, akidai kuwa hataogopa kuvunja mguu wa mpinzani wake, “yalikuwa yanaashiria kwamba badala ya kutekeleza makubaliano ya Arusha, angewaua wale waliotaka yatekelezwe.”
Aliendelea kusema:
“Pia hilo ndilo alilokuwa ametangaza tarehe 15 Novemba 1992 akiwa katika uwanja wa michezo wa Ruhengeri, kwenye mkutano wa chama cha MRND, alipowaambia Interahamwe kwamba wakati ukifika atawavika sare na watashuka kazini, akimaanisha kwenda kutekeleza mauaji ya kimbari.”
Waziri wa Umoja wa Wanyarwanda aliongeza kuwa wakati Habyarimana alipokuwa akitoa maneno hayo ya uchochezi huko Ruhengeri, Watutsi walikuwa wanauawa huko Kigali, katika Wilaya ya Shyorongi, wakiwemo wanawake na watoto. Pia nyumba zilikuwa zikibomolewa, hata za baadhi ya Wahutu waliokuwa hawakubaliani na MRND/CDR, na takriban watu 500 walibaki bila makazi.
Alisema kuwa wakati huo Habyarimana alipita eneo hilo akielekea nyumbani hadi Kigali.
Brightafrica
