Rais wa FERWAFA Shema : VAR kutoka Tanzania kufanyiwa majaribio kwenye ligi ya Rwanda
Na Christopher Karenzi
Rais wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA), Shema Fabrice, akiwa pamoja na Hadji Yussuf Mudaheranwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kuu ya Soka nchini Rwanda wamefanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Shirikisho la soka FERWAFA jijini Kigali, Jumatatu, tarehe 27 Oktoba 2025.
Kwenye Agenda ya Kikao, ilikuwa kuzungumza hasa juu ya Shirikisho la Soka kuthibitisha kuwa klabu za Al Hilal SC, Al Merrikh SC na El Ahli SC Wad Medani kutoka Sudan zitashiriki michuanao ya ligi ya soka ya Rwanda kuanzia wiki hii.
Ligi Kuu ya Rwanda msimu wa 2025/26 umefikia mzunguko wa tano, lakini habari kubwa kwa sasa ni kuhusu matatizo ya uamuzi, ambapo baadhi ya waamuzi wamesimamishwa na timu nyingi zimekuwa zikiwasilisha malalamiko.

Rais wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA), Shema Fabrice
Akiongea na vyombo vya habari Rais wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA), Shema Fabrice amesema kwamba wakati timu hizo ziliomba kushiriki katika Ligi Kuu ya Rwanda, ligi ya kwao haipo tena wakati huu kutokana na machafuko na usalama mdogo nchini Sudan, Shema aliwauliza kwanini wamependekeza kuja Rwanda. Walimjibu kwamba Rwanda inatambulika kwa kuwa na usalama wa hali ya juu, na pia walikuwa wamepata ushuhuda kutoka kwa raia wenzao wa Sudan wanaoishi nchini Rwanda.
Shema amesema: “Waliniambia kwamba Rwanda, kwa upande wa soka, bado haijulikani sana kimataifa, lakini kwa kiwango cha usalama ipo juu sana; kwa mapokezi mazuri ya wageni, hakuna tatizo la rushwa, na hata ushuhuda wa Wasudani wanaoishi hapa unaonyesha kwamba kila mtu anaishi vizuri na ana nyaraka halali zinazomtambulisha.”
Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa) Shema amefahamisha kwamba viwanja vya Gicumbi, Rutsiro na Rusizi vitakuwa tayari mwishoni mwa mwaka huu wa 2025, na vitaanza kutumika katika michezo ya marudiano, ili timu ambazo kwa sasa zinakodisha viwanja ziweze kurejea kuchezea nyumbani kwao.
Kuhusua mchakato wa kutumia Teknolojia ya VAR, amesema kwamba utaanza kufanyiwa majaribio huku waamuzi wakipewa mafunzo maalum, ili ifikapo msimu ujao wa mashindano Rwanda iweze kuanza kuitumia kikamilifu.
Kiongozi huyo alipoulizwa kuhusu changamoto za uamuzi ambazo zimekuwa zikionekana mara kwa mara katika ligi hasa baada ya baadhi ya waamuzi kusimamishwa kwa muda amesema:
“Katika ukanda wetu, kitengo cha VAR kiko nchini Tanzania, lakini niliwaambia kuwa si rahisi kutuma waamuzi wawili pekee kati ya mia mbili. Niliwaomba VAR kutoka Tanzania iweze kuja Rwanda ili tuweze kuwafundisha waamuzi wengi zaidi.”
Ameongeza:“Ikiwezekana, tunatarajia kuanza kuijaribu VAR katika michezo ya mzunguko wa kwanza, ili ifikapo mzunguko wa pili tuanze kuitumia rasmi. Na msimu ujao wa ligi tutaweza kuitekeleza ipasavyo.Ninachoweza kusema ni kwamba tupo katika mchakato wa mageuzi ya uamuzi, na kufikia Februari michezo ya mzunguko wa pili tutakuwa na VAR ikitusaidia. . Shema ameongeza
Hadji Yussuf Mudaheranwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kuu ya Soka nchini Rwanda ameelezea vyombo vya habari kuwa kwenye ligi ya soka sasa Timu zimefikia 19 kutoka 16, hakuna tatizo la kuwepo idadi hiyo
Amesema “ Kwenye michezo ya awali watacheza mechi za viporo, huku katika michezo ya marudiano ratiba itabdilika, Kila timu itakuwa na siku moja ya mapumziko katikati ya wiki. Mfano timu iliyocheza Ijumaa inaweza kurudi uwanjani tena Jumanne’’. Hadji Mudaheranwa

Hadji Yussuf Mudaheranwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi kuu ya Soka nchini Rwanda
Kuhusu suala la kutwaa taji la ubingwa wa ligi amesema ‘’ Mfano timu kutoka Sudan ikiwa labda imetawaza mabingwa watapewa kombe lao na kutafanyika sherehe za kuikabidhi kombe lakini pia timu ya Rwanda hata ikiwa ya 3 au 4 itakabidhiwa taji la ubingwa hapa nchini itasherehekea pia ushindi na itawakilisha Rwanda kwenye michuano ya Champions League wakati timu hiyo ya Sudan wao watawakilisha nchi yao vile vile’’
Katika mkutano na waandishi wa habari, walikuwepo pia wawakilishi wa Timu hizo kutoka Sudan zitakashiriki michuanao ya ligi ya soka ya Rwanda kuanzia wiki hii wakti viongozi wa vilabu hivyo wakisubiriwa nchini Rwanda siku za hivi karibuni.

Waandishi wa habari
