APR Handball Club  watawazwa mabingwa msimu 2025-26

Share Now

Na Christopher Karenzi

Timu ya  mpira wa mikono ya Handiboli  APR HB  wanaume wametawazwa mabingwa msimu huu wa 2025-26 nchini Rwanda  baada ya Kuwabwaga  wapinzani wao wakubwa, Police HC kwa ushindi wa magoli 31 kwa 29 katika ukumbi wa Petit Stade Amahoro uliopo Remera, jijini Kigal tarehe 30 Juni 2026.

APR HC ilihakikisha inanyakua taji hilo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 31 kwa 29 katika mchezo wa tano na wa mwisho wa fainali za play-offs, uliochezwa jioni ya tarehe 30 Juni katika ukumbi wa Petit Stade Amahoro uliopo Remera, mbele ya mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia pambano hilo.

Awali, Police HC ilikuwa imeanza vyema kwa kushinda michezo miwili ya kwanza kati ya mitano iliyopangwa. Hata hivyo, APR HC ilionyesha uthabiti mkubwa kwa kushinda michezo miwili iliyofuata na kusawazisha ushindi kuwa michezo miwili kwa miwili, kabla ya kuhitimisha kazi katika mchezo wa mwisho.

Kocha Mkuu wa APR Handball, Bagirishye Anaclet, ameonyesha furaha yake baada ya kuiongoza timu yake kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Akizungumza baada ya ushindi huo, alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio yaliyopatikana.

Alisema: Ninamshukuru Mwenyezi Mungu. Tangu kampeni ya ligi ilipoanza mwezi Oktoba 2025 hadi hatua za mtoano (Playoffs), safari haikuwa rahisi. Pia ninawashukuru viongozi wa timu yetu ambao walikuwa nasi bega kwa bega katika kipindi chote.”

Aliendelea kusema ”Tulipopoteza mechi mbili mfululizo, morali ya wachezaji ilishuka. Hata hivyo, viongozi waliwatia moyo na kuwahimiza wasikate tamaa. Walisisitiza kwamba tulipaswa kupambana hadi dakika ya mwisho. Wachezaji walionyesha moyo wa kujituma na kupambana hadi mwisho, jambo lililotuwezesha kutwaa ubingwa wa mwaka huu.”

Kocha Mkuu wa APR Handball, Bagirishye Anaclet,

Kwa upande wa Shirikisho la handboli nchini Rwanda, Rais wa shirikisho la mchezo wa Handiboli Alphred Twahirwa anaeleza  kuwa msimu huu ulikuwa mrefu “Naweza kusema kwamba ilikuwa safari ndefu. Ligi ilianza mwezi Oktoba mwaka uliopita. Kwa ujumla, ligi ilienda vizuri kwa sababu tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho kulikuwa na ushindani mkubwa. Mwanzoni tulianza kucheza mechi mikoani, baadaye tukahamia Kigali hadi kufikia hatua za mwisho za mashindano. Jambo jingine la kufurahisha ni kwamba mwitikio wa mashabiki ulikuwa mkubwa. Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa ligi ilifanyika kwa mafanikio.”

Rais wa FERWAFAND Alphred Twahirwa akikabidhi APR kombe la ushindi

Akizungumzia kuhusu  changamoto zilizojitokeza wakati wa mashindano hayo, Twahirwa alisema: Baadhi ya changamoto tulizokumbana nazo zilihusiana na uwezo wa kifedha wa baadhi ya timu. Pia, bado hazijafikia viwango tunavyotarajia katika ushiriki wao kwenye mashindano. Aidha, licha ya kuwa tuna miundombinu ya michezo, bado kuna baadhi ya viwanja, hasa vilivyoko mikoani, ambavyo haviko katika hali nzuri. Hilo pia ni changamoto kwa sababu baadhi ya viwanja havikidhi viwango vinavyohitajika.”

Wakhuka Bryan mchezaji wa zamani  wa Equit Bank ya Kenya, ni  miongoni mwa wachezaji waliofanikisha kwa  Club ya APR  Handiboli kutwaa ubingwa  msimu huu.

Akizungumza kuhusu ligi ya Rwanda amesema ‘’Ligi ya Rwanda kusema ukweli si rahisi na si ngumu unatakiwa utumie akili na nguvu’’

Mchezaji Bryan kushoto akikabiliana na wachezaji wa Police

Kijana huyo Amesema kuwa huu ni wakati wa kuendelea kujiandaa kwa sababu Clubbyake ya APR itawakilisha Rwanda kwenye michuano ijayo ya Kombe la mabingwa barani Afrika  octoba 2026 nchini Angola.

Kwa upande wa ligi ya Ligi Kuu ya Daraja la Kwanza  wanawake, E.SC. Nyamagabe ilitawazwa mabingwa baada ya kuifungaUR Rukara kwa mabao 40-23, huku Mutenderi TSSikitwaa ubingwa wa Ligi ya Daraja la Pili kwa wanaume kwa kuishinda TTC de la Sallekwa mabao 31-24.

Mabingwa APR HC

Kombe hili lililonyakuliwa  na APR HC ni la nne katika historia ya klabu hiyo, huku Police HC ikisaka ubingwa wake wa 11.

Kufuatia ushindi huo, APR HC itaiwakilisha Rwanda katika mashindano ya klabu bingwa za Afrika ya mpira wa mikono, Africa Handball Champions League 2026, yatakayofanyika nchini Angola mwaka huu.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *