Timu ya Taifa ya Rwanda ya mpira wa mikono kwa wanaume imeanza vizuri Kombe la Afrika linaloendelea jijini Kigali, baada ya kuifunga Zambia kwa mabao 30 kwa 19, Jumatano tarehe 21 Januari 2026, katika ukumbi wa BK Arena.
Na Christopher Karenzi
Hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo ya 27 yalizishirikisha mataifa 16 ya Afrika, yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na michezo.
Timu ya Taifa ya Rwanda, ilianza kwa kasi kubwa, hali iliyosababisha dakika 10 za mwanzo kumalizika ikiwa imeongoza kwa mabao 7 kwa 1.
Timu ya Zambia ilionyesha upinzani mzuri katika dakika zilizofuata, ikifunga mabao manne huku Rwanda ikifunga matano, na hivyo kumaliza dakika 10 za mwisho za kipindi cha kwanza matokeo yakiwa mabao 12 kwa 5.

Hafla ya ufunguzi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Michezo, Nelly Mukazayire Waziri wa Michezo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Mikono Afrika (CAHB), Dkt. Mansourou Aremou, pamoja na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Mikono nchini Rwanda, Twahirwa Alfred.

Waziri wa Michezo wa Rwanda Nelly Mukazayire
Katika matokeo mengine, Nigeria iliibwaga Algeria kwa magoli 25 kwa 23, Misri ikaifunga Gabon 36 kwa 25, Guinea iliichapa Kenya kwa magoli 36 kwa 27.
Aidha, Angola iliifunga Uganda kwa magoli 37 kwa 21. Mayanja Willy ni Kaimu Mwenyekiti wa Timu ya Taifa ya Uganda, amesema kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Uganda kushiriki mashindano ya kombe la Afrika. ‘’Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Uganda kushiriki mashindano haya. Bila shaka tulitarajia changamoto kubwa, lakini tuko tayari kuikabili. Tumejipanga kushiriki kikamilifu, kuendelea kujifunza na kuboresha maendeleo ya mchezo wa mpira wa mikono nchini Uganda’’.
Kwa matokeo mengine Morocco iliicharaza Benin 52 kwa 28, Cape Verde ikaifunga Congo Brazzaville 34 kwa 28, huku Tunisia ikiiinyeshea mvua ya magoli Cameroon 41 kwa 22. Michezo inafanyika kwenye viwanja vya BK Arena na Petit Stade, jijini Kigali.

Haya ndiyo makundi na timu zinakazoshiriki katika Mashindano ya Kombe la Afrika ya mpira wa mkono kwa wanaume ya mwaka 2026 yatakayofanyika mjini Kigali, Rwanda, kuanzia tarehe 21 hadi 31 Januari 2026:
Kundi A
· Rwanda
· Algeria
· Zambia
· Nigeria
Kundi B
· Uganda
· Gabon
· Angola
· Misri
Kundi C
· Kenya
· Cameroon
· Guinea
· Tunisia
Kundi D
· Benin
· Congo Brazzaville
· Morocco
· Cape Verde
