Share Now

Wajumbe kutoka nchi 24 wa Kijeshi, kutoka barani Afrika  wakutana jijini  Kigali                     

Na Christopher Karenzi

Rwanda imeeleza kuwa maarifa ya kutosha kwa wanajeshi wa Afrika  kuwa ndio msingi wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoikabili bara hilo.

Hayo yamezungumzwa Jumatatu tarehe 10 Novemba 2025 na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Juvenal Marizamunda, alipofungua rasmi mkutano wa siku tatu wa 19 wa Wakuu wa Vyuo vya Kijeshi barani Afrika (ACoC) unaofanyika mjini Kigali.

Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 24, wakuu wa vyuo vikuu vya kijeshi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wawakilishi wa Idara ya Usalama na Amani ya Umoja wa Afrika, wataalamu wa masuala ya kijeshi na wadau wengine, ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Mustakabali wa mafunzo na elimu ya kijeshi barani Afrika: Kuondoa pengo la kiteknolojia.”

Waziri Marizamunda amesisitiza kuwa maarifa ya kina kwa wanajeshi ndiyo silaha ya msingi katika kupambana na changamoto za kiusalama barani Afrika, ikiwemo mashambulizi yanayotumia teknolojia, uhalifu wa kuvuka mipaka, na changamoto nyinginezo. Amesema:“Changamoto zinazoikabili Afrika ni nyingi, zikiwemo ugaidi, uhalifu wa kuvuka mipaka, uhamiaji haramu, na mabadiliko ya tabianchi.
Kuzitatua kunahitaji wanajeshi walioelimika siyo tu katika masuala ya kijeshi, bali pia wanaofahamu teknolojia na wenye maadili mema. Hayo ndiyo msingi wa ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.”

Aidha, Waziri Marizamunda amehimiza nchi za Afrika kushirikiana kwa karibu zaidi, hususan kupitia vyuo vya kijeshi, na kuwataka washiriki wa mkutano huo kuwa na majadiliano yenye tija na kuhakikisha maazimio yatakayofikiwa yanatekelezwa.

Amepongeza mchango wa ACoC katika kuimarisha umoja na dira inayolenga mafunzo yenye mwelekeo wa Umoja wa Afrika na Jeshi la Dharura la Afrika (African Standby Force).

Kupitia mkutano huo, vyuo vya kijeshi vinabadilishana uzoefu na kutafuta mbinu za kuoanisha mitaala, hivyo kuimarisha ushirikiano wa kijeshi ndani ya Umoja wa Afrika.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Nyakinama, Brigedia Jenerali Andrew Nyamvumba, alieleza kuwa mkutano huo haukulenga tu kuwakutanisha washiriki, bali pia kubadilishana ujuzi na maarifa ya kijeshi.“Ni jukwaa la kukutanisha ujuzi na hekima ya kijeshi ya Afrika.” Ameongeza

Brigedia Jenerali Nyamvumba amefafanua kuwa katika kipindi cha siku tatu, washiriki watajadili changamoto kuu zinazoikabili taasisi za elimu ya kijeshi barani humo, ikiwemo uoanishaji wa mitaala, matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, na mbinu za kisasa za kujifunza.

Amesisitiza kuwa majadiliano hayo yatasaidia kuandaa kizazi kipya cha viongozi na watumishi wa majeshi walio tayari kuongoza vikosi vya pamoja na kukabiliana na changamoto za kiusalama za sasa na zijazo, kwa lengo la kujenga amani na usalama wa kudumu barani Afrika.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *