Share Now

Rais Kagame awaonya maafisa wa jeshi kujilinda pombe na dawa za kulevya

Na Christopher Karenzi

chriskarenzi@gmail.com

Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Rwanda (RDF), ametoa wito kwa maafisa wapya wa jeshi kuepuka matumizi ya pombe kupindukia na dawa za kulevya, akisema kuwa jukumu lao ni kulilinda taifa na kuhakikisha usalama wa kutosha kwa wananchi.

Rais Kagame ametoa kauli hiyo  Ijumaa, tarehe 3 Oktoba 2025, katika Chuo cha Kijeshi cha Gako, wilaya ya Bugesera katika jimbo la Mashariki wakati wa hafla ya kuwapa vyeo na kuwapokea rasmi maafisa wapya 1,029 waliohitimu mafunzo na kujiunga na Jeshi la Rwanda (RDF).

Maafisa hao ni wa kundi la 12 la waliohitimu katika chuo hicho, wakiwemo 557 waliohudhuria mafunzo ya mwaka mmoja, 248 wa mafunzo ya muda mfupi, 182 waliohitimu mafunzo ya miaka minne, na 42 waliopata mafunzo yao katika  vyuo vya  kijeshi nje ya Rwanda.

Katika hotuba yake, Rais Kagame amewapongeza kwa bidii na moyo waliouonyesha wakati wa mafunzo magumu waliyoyapitia na kuwashukuru wakufunzi wao kwa mchango wao mkubwa katika kuwaandaa.

Amesema: “Nawashukuru wale waliowafundisha kwa mchango mkubwa walioutoa kuwaandaa ili nanyi muweze kutekeleza majukumu yenu ipasavyo. Pia tunashukuru nchi rafiki ambazo tulishirikiana nazo katika elimu na mafunzo mliyoyapata.”

Rais Kagame pia aliwashukuru wazazi wa maafisa hao kwa kuwaunga mkono watoto wao waliamua kuingia katika taaluma ya heshima.

Aliwakumbusha kuwa jukumu walilopewa la kulinda Rwanda na raia wake ni la heshima kubwa na wanapaswa kulitekeleza kwa uadilifu na uzalendo.

“Tunataka mlihifadhi taifa la Rwanda, wananchi wake na wote wanaoishi humo… Jukumu lenu ni kuhakikisha nchi ina usalama wa kutosha, isivamiwe na wale wasiotakia mema taifa letu.”

Rais Kagame akikagua gwaride la Maafisa wapya

Amesisitiza kuwa mchango wao katika ujenzi wa taifa unahitaji kujitolea, nidhamu, na uelewa wa mabadiliko yanayotokea duniani, akisema kuwa wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto yoyote.

“Sasa mmekuwa sehemu ya wale wanaojaribiwa; dunia inabadilika na inaweza kuelekea pabaya – msiende huko, endeleeni kuwa kwenye njia inayofaa, njia inayofaa kwa ajili ya Rwanda. Kitu chochote kitakachotishia hiyo njia kinapaswa kupingwa, na mafunzo mliyoyapitia yamewapa uwezo wa kushinda mitihani hiyo.” Amesema  Rais Kagame

Aidha amewaasa kuhusu mienendo mibaya, kujiepusha na ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

“Jiepusheni na ulevi wa kupindukia – mambo ya kunywa pombe hadi kupoteza mwelekeo. Ukishapoteza mwelekeo, unapoteza kazi zako na majukumu mliyokula kiapo kuyatekeleza. Dawa za kulevya huondoa akili – na mtu asiye na akili timamu hawezi kutimiza majukumu yake.”

Shule Kuu ya Kijeshi ya Gako, imekuwa ikitoa mafunzo ya maafisa wa jeshi kwa miaka 25, ikiandaa maafisa kutoka Rwanda na mataifa mengine rafiki yanayowapeleka wanafunzi wao kupata elimu ya kijeshi nchini humo.


Share Now

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *